Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ombi rasmi la Algeria kujiunga na kundi la BRICS

Algeria Yatuma Maombi Ya Kujiunga Na BRICS Ombi rasmi la Algeria kujiunga na kundi la BRICS

Mon, 24 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika muendelezo wa harakati ya nchi mbalimbali duniani kuelekea kwenye miungano na mashirika yasiyo ya Magharibi, Rais wa Jamhuri ya Algeria, Abdelmadjid Tebboune, amewasilisha rasmi ombi la kutaka nchi hiyo ijiunge na kundi la BRICS na kutoa wito wa kuimarishwa uhusiano wa kibiashara na ushirikiano wa kiuchumi na Russia na nchi wanachama wa kundi hilo.

Moussa Kharfi, Naibu Spika wa Bunge la Algeria amesema: Iwapo Algeria itajiunga na kundi la BRICS, nchi za Afrika zitanufaika na suala hili katika nyanja nyingi.

Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune Maombi ya uanachama katika kundi la BRICS ambalo Russia na China ni miongoni mwa wanachama wake wakuu, yamezidi kuwa muhimu katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya vita vya Russia na Ukraine na hatua za Marekani na washirika wake ya kuiunga mkono Kiev katika vita hivyo.

BRICS ni jina la kundi linaloongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani, ambalo linaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Kundi hili lilianzishwa mwaka 2009 katika fremu ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi wanachama kwa lengo la kukomesha utegemezi kwa sarafu ya dola ya Marekani. Sasa, baada ya takribani miaka 14 tangu kuundwa kwa kundi hilo, nchi nyingi zimeomba uanachama katika jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, Misri, Argentina na Uturuki.

Anil Sooklal, mwakilishi wa Afrika Kusini katika kundi la BRICS, amesema katika muktadha huo kwamba, nchi 19 zimeomba kujiunga na BRICS. Kundi hili la BRICS lina uwezo mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya haraka ya kiuchumi na kuwa nguzo yenye ushawishi na maamuzi katika uchumi wa kimataifa. Kwa upande mwingine, hatua za Marekani na waitifaki wake na kutumia sarafu ya dola kama chombo cha kuzishinikiza nchi mbalimbali ili zitii na kufuata sera za Marekani kumezifanya nchi hizo kuchukua maamuzi ya kuomba uanachama katika kambi hiyo ya kiuchumi. Vladimir Putin, Rais wa Russia amesisitiza katika muktadha huu kwamba, nchi za BRICS zinapaswa kushirikiana katika kukomesha dosari za mfumo wa fedha duniani na kufutilia mbali ulazima wa kutumia sarafu maalumu hususan dola ya Marekani kwa ajili ya miamala ya kibiashara na akiba ya kigeni.

Kwa hakika, kujiunga na BRICS kunazipa nchi mbalimbali uwezo wa kupunguza udhibiti na utawala wa dola kwenye uchumi wa dunia na kutayarisha uwanja mzuri wa ustawi wa kiuchumi kwa njia ya mabadilishano ya biashara na ushirikiano wa kiuchumi kwa muda mfupi baina ya nchi zenye mitazamo na mwelekeo sawa.

Ma Zhaoxu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya China anasema kuhusiana na suala hili kwamba: China pamoja na nchi wanachama wa BRICS ziko tayari kuimarisha mshikamano na mshikamanio na nchi zinazoendelea na zile zinazoinukia kiuchumi.

BRICS inafanya jitihada za kuwa chombo kikubwa na chenye nguvu zaidi cha kisiasa na kiuchumi "kisio cha Magharibi" ambacho kinaweza kupambana na dola ya Marekani na utawala wa sarafu za Magharibi. Katika mkondo huu nchi nyingi duniani zimeonyesha hamu ya kushirikiana na BRICS.

Leonid Slutsky, Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Duma ya Russia, anasema: "BRICS itatimua kivumbi na kuacha nyuma ulimwengu wa kambi moja unaoongozwa na Marekani na kukomesha udhibiti wa sarafu ya dola. Dunia haitaki kabisa kuwa mateka wa sera ya uchokozi ya Marekani."

Ombi la Algeria la kujiunga na BRICS na foleni ya nchi nyingine zinazotaka kujiunga na jumuiya hiyo vinaweza kutathminiwa katika mkondo huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live