Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameitaka Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kuiokoa nchi hiyo kutokana na "hatari inayokuja" kutokana na kile alichokitaja kuwa ufisadi wa mchakato wa uchaguzi.
Katika taarifa yake, alisema mvutano unaongezeka na akimtaka Rais Buhari Muhammadu, "acha chaguzi zote ambazo hazijapitisha mtihani wa uaminifu na uwazi zifutwe".
Alisema uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (Inic) kurejea katika matumizi ya utumaji matokeo kwa mikono ulifanyika kwa makusudi licha ya kutumia fedha nyingi kuanzisha mfumo wa kielektroniki utakaoruhusu utumaji wa matokeo mara moja kutoka katika vituo vya kupigia kura.
"Sio siri kwamba maofisa wa INEC, katika ngazi ya uendeshaji, wamehujumiwa ili kufanya kile ambacho kingefanya kazi kisifanye kazi na kurejea uwasilishaji wa matokeo kwa mikono ambao huchezewa na matokeo kuthibitishwa," alisema.
Rais huyo mstaafu pia alitoa wito kwa wananchi kuwa na subira na kueleza imani na "mfumo wa kufanya kazi kwa haki". "Ninaamini kabisa kwamba hakuna mtu atakayecheza na mustakabali wa Nigeria katika wakati huu," alisema.