Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisi ya kiongozi rasmi wa upinzani yapendekezwa Kenya

Ofisi Ya Kiongozi Rasmi Wa Upinzani Yapendekezwa Kenya Ofisi ya kiongozi rasmi wa upinzani yapendekezwa Kenya

Mon, 27 Nov 2023 Chanzo: Bbc

Kamati ya mazungumzo ya kitaifa yaliyohusisha serikali na muungano wa upinzani Kenya imetoa ripoti yake mwishoni mwa juma ambapo pande hizo mbili zimefikia masuala kadhaa yaliyokuwa yanasababisha mikwaruzano ya kisiasa nchini humo.

Baadhi ya mambo yaliyofikiwa ni pendekezo la kuundwa kwa wadhifa wa Waziri mkuu na ofisi ya kiongozi rasmi wa upinzani na manaibu wake wawili.

Rais wa Kenya William Ruto amesema atatekeleza mapendekezo makuu ya ripoti hiyo hiyo ya mwisho ya kamati ya mdahalo wa kitaifa ijulikanayo NADCO ambapo imeitaka serikali kupunguza safari za maafisa wa serikali kwa asilimia hamsini,akisisitiza kuhusiana na suala hilo la kupunguza safari ameshafanya hivyo.

Ruto ameahidi kuwa mapendekezo ya kamati hiyo yanayogusia uongozi yatatekelezwa akiitaja ripoti hiyo kama nzuri kwa nchi.

Ameongeza kuwa ni wajibu wa wabunge sasa kuijadili ripoti hiyo iliyowasilishwa na viongozi wa kamati hiyo,kiongozi wa walio wengi bungeni Kimani Ichung'wa na kiongozi wa upinzani katika mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka akisema ni muda wa kusonga mbele pamoja kama taifa.

Haya hivyo mapendekezo hayo yaliyolenga kutuliza joto la kisiasa Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka uliopita,hayaungwi mkono na vinara wote wa upinzani. Kiongozi wa chama cha DAP Kenya Eugene Wamalwa amejitenga na ripoti hiyo licha ya kuwa alikuwa sehemu ya viongozi walioketi kuyajadili masuala hayo katika kamatu hiyo ya mdahalo wa kitaifa.

Bwana Wamalwa anasema suala la kupunguza gharama ya maisha kuwapunguzia raia wa kawaida makali ya mfumko wa bei na kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu halikupewa uzingativu uliostahili.

Hoja kuu ya upinzani kutaka kuwepo kwa mazungumzo na serikali baada ya uchaguzi ilikuwa ni kujadili namna ya kupunguza gharama ya maisha,suala ambalo lilisababisha upinzani ukiongozwa na Raila Odinga kuitisha mara kadhaa maandamano ya umma kuishinikiza serikali kushughulikia tatizo hilo.

Kiongozi mwingine anayeripotiwa kupinga mapendekzeo ya NADCO ni Bi Martha Karua,kiongozi wa chama cha NARC Kenya,aliyekuwa mgombea mwenza wa Bwana Odinga katika uchaguzi wa Rais.

Kupitia ukurasa wake wa X,Bi karua amesema kuidhinisha makubaliano yoyote yasioangazia masuala muhimu kama kupanda kwa gharama ya maisha,mfumo wa uchaguzi na demokrasia ya vyama vingi ni kuwatapeli Wakenya na yanapaswa kupingwa.

Haijabanika wazi msimamo wa kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga kuhusu mapendekezo hayo ya kamati ya mdahalo wa kitaifa NADCO ambayo wakosoaji wake wanaufananisha na mpango wa maridhiano ya kitaifa BBI uliopingwa katika utawala uliopita.

Chanzo: Bbc