Kiongozi wa ODM Raila Odinga ameahidi kutunza familia ya aliyekuwa mlinzi wa mkewe Ida, marehemu Barack Oduor,ambaye aliuawa kwa risasi mapema mwezi huu.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Oduor siku ya Ijumaa, kiongozi huyo wa upinzani aliahidi kuhakikisha kwamba mahitaji ya wanafamilia wa karibu wa marehemu yanazingatiwa.
Raila alisema atahakikisha watoto wa afisa huyo wa polisi aliyeaga wanapata elimu hadi kumaliza.
“Barack ameacha mke mdogo, ana watoto wadogo sana, naahidi kumtunza mke wake na watoto, tutawasomesha hadi watakapomaliza masomo yao,” alisema.
Oduor alikata roho mnamo Oktoba 14 baada ya kupigwa risasi na mshambuliaji huko mtaa wa Riat, Kisumu Magharibi.
Collins Okundi, meneja wa Klabu moja mjini Kisumu, anadaiwa kumpiga risasi na kumuua Otieno baada ya kuzozana na tayari amekamatwa na kufikishwa mahakamani.
"Walipofika eneo la Estate,Collins Okundi, Meneja wa Club Signature jijini Kisumu alitokea ghafla na kukazuka mzozo kati ya aliyeandikisha taarifa, Donar Kajwang na Cpl Barrack Otieno Oduor. Katika harakati hizo, Collins Okundi alimpokonya bunduki afisa huyo wa polisi na kumuua kwa kumpiga risasi mbili kwenye kichwa na mguu. Donar Kajwang alipigwa risasi ya mguu na kukimbizwa katika hospitali ya Aga khan Kisumu na yuko katika hali nzuri," sehemu ya ripoti ya ilisoma.
Baada ya tukio hilo,Bi Ida alilaumu matumizi mabaya ya dawa za kulevya, akisema vijana walikuwa na wakipandwa na hasira haraka.
Mkewe Raila alimwombolezea marehemu, akisema alikuwa mtu mwema. Alisema vijana wengi wamejiingiza katika ulevi na bangi, na hivyo kusababisha maamuzi yasiyo sahihi maishani.
"Hasira ni hasara. Si lazima umuue mtu kwa sababu kuna mtu amemsalimia mpenzi wako," Ida alisema wakati wa maziko huko Bondo.
Pombe na bangi haziwezi kujenga taifa, alisema. Alieleza kuwa vijana wamepotea katika matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
"Pombe zilikuwa zikinywewa na wazee kwenye viunga vyao vya kuvizia nyakati za jioni wakati bangi ilikuwa kitu cha wagonjwa wa akili. Vijana, kuwa makini. Epuka matumizi ya dawa za kulevya," Ida alisema