Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anazuru hospitali kuangalia watu waliojeruhiwa na polisi wakati wa maandamano ya hivi majuzi.
Baadaye atakuwa akifanya mkesha kwa waliouawa katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyofanyika kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.
Kulingana na mashirika ya kutetea haki za binadamu, takriban watu 30 wamefariki katika mji mkuu, Nairobi, na miji mingine kote nchini.
Wamekosoa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi, lakini wizara ya mambo ya ndani imetetea hatua za maafisa.
Bw Odinga alisitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika wiki hii kwa sababu ya vifo hivyo na atakuwa akiwasha mishumaa na kuweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu yao.
Kwa mara ya kwanza aliitisha misururu ya mikutano mwezi Machi.
Pande hizo mbili zilikubaliana kufanya mazungumzo, lakini upinzani ulisema timu ya Rais William Ruto haikujitolea kusuluhisha malalamishi yao.
Kisha mwezi uliopita, Bw Ruto alitia saini mswada tata wa fedha ulioongeza maradufu ushuru wa mafuta na kuanzisha ushuru mpya wa nyumba miongoni mwa hatua zingine ambazo zimechukuliwa kuwa za ukandamizaji.
Hii ilisababisha maandamano ya hivi punde. Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanadiplomasia wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu hali nchini Kenya, wakiitaka serikali na upinzani kutatua tofauti zao kwa amani.
Rais sasa ameeleza nia yake ya kukutana na kiongozi huyo wa upinzani, akiandika kwenye Twitter: "Rafiki yangu @RailaOdinga, naenda Tanzania... Nitarejea [Jumatano] jioni, na kama ujuavyo siku zote,' ninapatikana.