Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Odinga: Kilichofanyika uchaguzii Kenya ni dhuluma, sitanyamaza

Dhuluma Odinga Odinga: Kilichofanyika uchaguzii Kenya ni dhuluma, sitanyamaza

Wed, 24 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 9, 2022, Raila Odinga amesema haogopi wala hatatetereka kusimamia haki na kuwatetea Wakenya dhidi ya watu wanaoendekeza ufisadi na wizi.

Odinga ambaye katika matokeo ya kura za urais zilizotangazwa Agosti, 15, 2022 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, alishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.9 akitanguliwa na William Ruto aliyepata kura milioni 7.1.

Hata hivyo tayari Odinga amefungua kesi ya kupinga ushindi wa Ruto katika Mahakama ya Juu ya Milimani ambayo inaendelea kukusanya vielelezo vya shauri hilo kutoka pande zote zinazohusika.

Akiwa kwenye mkutano na wajumbe wa Azimio la Umoja, uliofanyika jijini Mombasa, leo Jumatano, Agosti 24, 2022, Odinga amesema kilichofanyika katika Uchaguzi Mkuu ni dhuluma kwa Wakenya hivyo hatokubali kunyamazia vitendo hivyo.

“Sina woga wala huruma kwa wanaofanya ufisadi, naamini siku chache zijazo watu wengi watajua ukweli. Yale tuliyoyaona ni machafu sana, sisi tunapambana na ufisadi na hata tukirudi kwenye uchaguzi tutashinda tu” amesema

Huku akishangiliwa na wajumbe waliokuwapo kwenye mkutano huo uliolenga kuhamasisha mipango ya kumsaidia mgombea wa ugavana katika Kaunti ya Mombasa, Abdulswamad Nassir ashinde katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 29 mwaka huu, Odinga amesema anaamini Mahakama ya Juu itawafichua walioiba kura

Odinga amesema kuna watu wanawanunua wanasiasa wenzao ili waonekane wana nguvu zaidi lakini wanajua hawana isipokuwa walifanya hila kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa IEBC ndiyo wakatangazwa washindi.

“Chebukati haoni aibu, amefanya mambo yasiyofaa na hii si haki. Hivi sasa amebaki peke yake, anapaswa akae kando ili haki iweze kutendeka” amesema

Odinga pia amewataka Wakenya wasife moyo kwa kilichotokea bali wajitokeze kwa wingi kumpigia kura Nassir ili kuwaonyesha watu Azimio la Umoja wanavyokubalika.

Naye mgombea mwenza, Martha Karua amesema Odinga ni mfano wa kuigwa kwa kuwa hachoki kuwatetea Waenya na kama ingekuwa mtu wa kawaida kwa yale aliyopitia Odinga angechoka na kukataa tamaa

“Amesimama wima na Wakenya, Mungu aendelee kumtunza na tumshikilie hivyo hivyo, siku ya kupata haki ipo karibu na tutapata haki yetu, kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa mapishi’ amesema Karua

Chanzo: Mwananchi