Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amekana kufanya mazungumzo ya mapatano ya kisiasa na Rais William Ruto katika mikutano yao mitatu mwishoni mwa juma.
Bw Odinga mnamo Jumanne alitaja mkutano wake na Rais Ruto katika mazishi katikati mwa kaunti ya Nyandarua na baadaye katika mechi mbili za kandanda za mashinani kama "mikutano ya bahati nasibu" ambayo haikuwa na uhusiano wowote na hali ya kisiasa nchini.
Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya mnamo 2018 aliingia katika makubaliano ya baada ya uchaguzi maarufu "handshake" na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Amekuwa akishambuliwa mara kwa mara na utawala wa Kenya Kwanza kwamba maandamano yake dhidi ya serikali yalikuwa ni mpango wa kulazimisha ''handshake'' na Rais Ruto.
"Hatukuzungumzia lingine lolote zaidi ya soka. Naomba ifahamike kwamba, hatutaki kushirikiana na serikali na hatujaomba," Bw Odinga alisema.
Mikutano hiyo mitatu kati ya rais na waziri mkuu huyo wa zamani ilikuwa imezua tetesi za kuwepo kwa mapatano ya kisiasa kati ya wapinzani hao wawili.
Pande zote mbili zilishiriki picha za Rais Ruto na Bw Odinga wakiwa wamekaa karibu, wakifuatilia mechi za soka kwa moyo mkunjufu.
Haya yanajiri huku Bw Odinga akitishia kuitisha maandamano mapya kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 unaopendekeza Wakenya kutozwa ushuru zaidi.