Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OCHA kukabiliana na manyanyaso ya kijinsia DRC

OCHA Kukabiliana Na Manyanyaso Ya Kijinsia DRC OCHA kukabiliana na manyanyaso ya kijinsia DRC

Wed, 6 Dec 2023 Chanzo: Voa

Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu, OCHA, limesema kuwa linafanya kazi na mashirika mengine ya kibinadamu ili kusaidia kupunguza na kukabiliana na ongezeko la matukio ya unyanyasaji wa kijinsia huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Naibu mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa DRC, Suzanna Tkalec, alisema siku ya Jumatatu mjini Washington kuwa wanawake na wasichana katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri wanaendelea kukabiliwa na viwango vya kutisha vya ukatili wa kijinsia kutokana na kuzuka upya kwa vurugu kati ya makundi ya wapiganaji na vikosi vya serikali.

Tkalec alisema ripoti ya hivi karibuni ya shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka iligundua kuwa wanawake na wasichana wapatao 90,000 walitafuta msaada wa matibabu baada ya kushambuliwa na kubakwa mwaka huu. Ripoti hiyo ilisema huenda waliojitokeza wanawasilisha sehemu ndogo tu ya jumla ya waathirika.

Tkalec anasema manusura hawana uwezo wa kuzifikia huduma za uokoaji maisha za unyanyasaji wa kijinsia au kuripoti unyanyasaji wao, wakihofia kunyanyapaliwa na jamii zao au wahalifu kulipiza kisasi.

"Mengi ya matukio haya ni ya kweli, kutokana na mazingira magumu wanayoishi wanawake na wasichana," Tkalec alisema.

Anasema OCHA haina uwezo mkubwa wa kutoa msaada kwa sababu mpango wake wa kukabiliana na masuala ya kibinadamu kwa mwaka 2023 unafadhiliwa kwa asilimia 38 tu.

Chanzo: Voa