Matiang'i alisema hakuna sheria ambayo inatambua Karen kama Ikulu ndogo na hivyo haifai kulindwa na GSUAkiongea mbele ya kamati ya bunge Jumatano Septemba 1 alisema walifuata sheria katika kuwaondoa GSU Karen.
Matiang'i alitumia nafasi hiyo kumwanika DP Ruto akisema ni mmoja wa maafisa wa serikali wanaolindwa pakubwa.
Karen ni nyumbani kwa naibu rais William Ruto na wala si Ikulu au Ikulu ndogo kulindwa na maafisa wa kikosi cha GSU, Waziri Fred Matiang'i amesema.
Akiongea mbele ya kamati ya bunge kuhusu usalama wa kitaifa, Matiang'i alisema sheria haitambui Karen kama Ikulu ndogo.
Alisema hakuna sheria ambayo inasema Karen kuwe na maafisa wa GSU kama wanavyodai baadhi ya wandani wa DP Ruto.
"Nyumba ya DP Ruto si Ikulu au Ikulu ndogo, sheria ni wazi kuwa hapo ni nyumbani kwake. Sisi katika idara ya usalama hatufanyi kazi kumpendeza yeyote, tunafanya kile kinafaa," alisema Matiang'i.
"Nionyesheni sheria ambayo inasema nyumbani kwa naibu rais ni ikulu au Ikulu ndogo. Nionyesheni hiyo sheria na nitaichapisha kesho kwenye gazeti rasmi la serikali," Matiang'i alisema.
Wandani wa DP Ruto wamekuwa wakisema Matiang'i na mkuu wa polisi Hillary Mutyambai walivunja sheria kwa kuwaondoa maafisa wa GSU kutoka Karen.
Mwakilishi wa kina mama kaunti ya Uasin Gishu Gladys Shollei Agosti 26 alitishia kufika mahakamani kumshtaki Matiang'i.
Kuondolewa kwa maafisa hao wa GSU kutoka Karen kumezua joto la kisiasa ambalo lilimlazimu Matiang'i kufika bungeni kuelezea.
DP Ruto hata hivyo amewataka wandani wake kukoma mjadala wa suala hilo akisema hauna manufaa yoyote kwa Wakenya.
Ruto alisema yuko sawa kulindwa na maafisa kutoka kikosi cha AP na kuwatambua kama walio na ujuzi wa kutosha kuhakikisha usalama wake.