Kimya kirefu cha Rais Uhuru Kenyatta kimewatia wasiwasi wandani wa Rais mteule William Ruto, huku wakimsukuma kiongozi wa taifa atambue ushindi wa kinara wao.
Tangu Agosti 15, 2022 mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alipomtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi katika kinyang’anyiro cha urais, Rais Kenyatta hajatoa taarifa yoyote kuhusu ushindi huo.
Ilitarajiwa kuwa, kama Rais anayeondoka, angemtumia Dkt Ruto ujumbe wa pongezi walivyofanya watangulizi wake, Hayati Daniel Moi na Mwai Kibaki.
Lakini hata baada ya mgombea urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, kukataa kutambua ushindi wa Dkt Ruto na kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu, viongozi wa Kenya Kwanza wameendelea kushinikiza Rais Kenyatta atamtumbue kama mshindi halali.
Naibu Rais Mteule Rigathi Gachagua, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na Mbunge mteule wa Kiharu Ndindi Nyoro ni miongoni mwa wale ambao wamemtaka Rais Kenyatta kumpongeza Dkt Ruto “kuashiria uungwana.’
“Mpaka sasa, Rais Kenyatta hajazungumza na Rais mteule Ruto. Hata hivyo, hatutamlazimisha kutupongeza,” Bw Gachagua akasema juzi akiwa Nyeri.
“Lakini ikiwa ataendelea kunyamaza, ajue kwamba sherehe ya kumwapisha Ruto itaendelea bila shida yoyote. Siku hiyo hatutahitaji upanga, kile tutahitaji ni Biblia, nakala ya Katiba na Msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi,” akaongeza.
Kwa upande wake, Bw Wetang’ula anasema Rais Kenyatta anafaa kuonyesha “ukomavu” kwa kumpongeza Dkt Ruto kufuatia ushindi wake.
“Hata hivyo, kunyamaza kwa Rais Kenyatta sio jambo geni kwa sababu hata aliyekuwa Rais wa Amerika Donald Trump alidinda kumpongeza Joe Biden baada ya ushindi wake katika uchaguzi wa 2022,” akasema Jumamosi wiki jana alipohudhuria hafla moja ya mazishi katika eneo bunge la Kanduyi, kaunti ya Bungoma.
Bw Wetang’ula alisisitiza kuwa, Dkt Ruto atamhakikishia usalama Rais Kenyatta atakapostaafu na kumpa kazi ya kimataifa.
“Tutakupa kazi ya balozi wa heri njema ambapo utapata fursa ya kuhudumu nje ya nchi kutekeleza majukumu kama vile kuangalia chaguzi katika mataifa ya kigeni wanavyofanya marais wastaafu,” Bw Wetang’ula akasema.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Masibo Lumala anasema kimya cha Rais Kenyatta bila shaka kinaonyesha kuwa hakufuhia ushindi wa Dkt Ruto.
“Vile vile, Rais Kenyatta amejipata njia panda kuhusu suala hilo kwa sababu kando na kuwa Rais wa nchi, yeye ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio, muungano ambao mgombeaji wake wa urais Bw Odinga ni miongoni mwa wale waliowasilisha kesi katika Mahakama ya Juu kupinga ushindi wa Dkt Ruto,” anasema Dkt Lumala.
Hata hivyo, msomi huyo anasema kuna uwezekano mkubwa kwamba Rais Kenyatta anasubiri matokeo ya kesi iliyoko katika Mahakama ya Juu kabla ya kutoa kauli yake kuhusu matokeo hayo.
“Aidha, huenda hii ndio maana wiki jana, Rais Kenyatta alichelea kulizungumzia suala hilo alipokutana na viongozi wa kidini na wageni kutoka Amerika,” Dkt Lumala anaongeza.
Mnamo Alhamisi wiki jana, Rais Kenyatta aliwahakikishia viongozi wa kidini kwamba shughuli ya upokezaji mamlaka itaendeshwa “vizuri”.
Kando na unyamavu wa Rais Kenyatta, duru zinasema kuna uwezekano mkubwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati hajawasilisha nakala ya cheti cha ushindi ambacho alimkabidhi Dkt Ruto mnamo Agosti 15 Bomas of Kenya.
Imekuwa ada kwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kuwasilisha nakala za cheti cha mshindi wa uchaguzi wa urais kwa Rais anayeondoka na Jaji Mkuu.
Jambo jingine ambalo linawapa viongozi wa Kenya Kwanza wasiwasi ni kwamba, Kamati ya Kusimamia Upokezaji wa Mamlaka nayo imekimya kwa kipindi kirefu.
Kamati hiyo, inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, haijatoa taarifa kwa taifa kuhusu maandalizi yake.
Hii ni licha ya mrengo wa Kenya Kwanza kuteua wawakilishi wanne kujiunga na kamati hiyo ambayo imekuwa ikikutana katika Afisi ya Rais.
Wao ni; Spika wa Bunge Justin Muturi, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina, Mbunge Mwakilishi wa Kike Uasin Gishu Gladys Boss Shollei na Mkuu wa Wafanyakazi katika afisi ya Naibu Rais Davis Chirchir.