Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nigeria yakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha

NAIRA WEB Nigeria yakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha

Tue, 14 Feb 2023 Chanzo: BBC

Watu nchini Nigeria wameanza kulala nje ya benki. Wanataka kuwa wa kwanza kwenye foleni ili kupata hela kutoka kwa mashine ya pesa (ATM) pindi zinapowekwa asubuhi.

Ukosefu wa noti mpya ya naira umesababisha uhaba wa pesa huku wale ambao wanataka kubadilisha pesa zao wakijawa na wasiwasi katika nchi ambayo 40% ya watu hawana akaunti za benki.

Mahakama ya Juu Zaidi imeingilia kati suala hilo na imeamuru kwamba tarehe ya mwisho ya kubadilisha noti za zamani uongezwe lakini hatua hiyo haijasaidia.

Watu hapa kwa muda mrefu wamezoea matatizo ya mara kwa mara ya uhaba wa mafuta inayosababisha milolongo mirefu ya magari kutoka kwa vituo vya mafuta. Lakini sasa kuona misururu mirefu ya watu waliochanganyikiwa, na wenye hasira imekuwa jambo la kawaida nje ya benki huku nchi ikijiandaa kwa uchaguzi wa urais mwishoni mwa mwezi.

"Sijakula leo," anasema Abraham Osundiran, 36, wakati anasimama katika moja ya foleni mbili katika benki huko Ikoyi, ambayo ni kitovu kikuu cha biashara mjini, Lagos.

Kwa siku ya pili amelazimika kukosa kwenda kazini katika kampuni ya ujenzi kwa kwa sababu hana pesa taslimu ya kulipa nauli ya teksi. Baadhi ya Wanigeria wamegeukia malipo ya kidijitali, lakini wengi bado wanategemea sana pesa taslimu.

"Sina pesa taslimu. Nimelazimika kuachana na kifungua kinywa ili nije hapa, na sijui nitakula nini kwa siku iliyosalia."

Hali kama hiyo inawakabili watu wengi nchini humo.

Lilian Ineh amegundua kuwa watu wachache wanakuja kwenye saluni yake

"Inaumiza. Siwezi kwenda sokoni kwa sababu wanataka pesa. Magari ya usafiri wa umma pia yanataka pesa - sasa sina budi kutembea kwenda kila mahali," mfanyabiasha wa Lilian Ineh, 26, aliambia BBC katika saluni yake.

"Hakuna pesa za kununua bidhaa, kwa hivyo nina bidhaa chache za kuuza. Kuna wateja wachache zaidi. Kawaida siku ya Jumamosi huwa na angalau watano."

Jumamosi iliyopita, nilipata wateja wawili tu.

Raia wa Nigeria waliambiwa Oktoba mwaka jana kwamba noti za zamani zitabadilishwa na kuhimizwa kuweka akiba yoyote ya fedha katika benki.

"Walitufanya tuweke pesa zetu zote kwenye akaunti zetu, na sasa hatuwezi kuzipata. Ni dhiki," anasema Osarenoma Kolawole, 40. Anafanya kazi sekta ya uuzaji wa simu, lakini hajaweza kupata mshahara wake tangu alipolipwa wiki iliyopita. .

"Mara ya mwisho nilipoenda madukani, ilinibidi ninunue mayai badala ya samaki - ambayo iliniumiza sana - sio kwamba sio chakula, lakini kununua kile ambacho sikutaka, kwa sababu benki haziniwezeshi kufikia pesa zangu."

Benki Kuu ya Nigeria (CBN) ilisema kuwa ilibuni upya noti - naira 200, 500 na 1,000 - kuchukua nafasi ya fedha chafu zinazozunguka, kukabiliana na mfumuko wa bei, kudhibiti bidhaa ghushi na kukuza jamii isiyo na pesa.

Ilitumai hatua hiyo mpya ingeisaidia kupata baadhi ya pesa zilizohifadhiwa na watu binafsi na makampuni kwenye mfumo wa kifedha.

Mageuzi yamesababisha jamii isiyo na pesa - jambo ambalo CBN haikutarajia.

Watu wamekuwa wakipata ugumu wa kufanya malipo na na hata uhamisho wa fedha mtandaoni. Wachambuzi wanasema miundombinu ya kusaidia mfumo wa kidijitali si imara vilivyo.

"Wazo zima lilikuwa kupunguza ni kiasi gani cha pesa ambacho watu wanaweza kupata, ili kuwahimiza kufanya malipo ya kidijitali, ili [CBN] iweze kufuatilia pesa zinakwenda wapi," anasema Paul Alaje, mwanauchumi mkuu katika washauri wa usimamizi wa SPM Professionals.

"Lakini benki za Nigeria hazina uwezo au muundo wa kufanya malipo ya kidijitali kufanya kazi bila matatizo."

CBN haijasema ikiwa uhaba huo ni wa makusudi.

"Serikali imekuwa ikijaribu kuingiza nchi katika uchumi ambao hautumii fedha taslimu kwa miaka mingi," anasema mchambuzi wa sera na mwanauchumi Yemi Makinde.

"Nia yake ni nzuri, lakini haiwezekani, mifumo ya benki haikuwa tayari na Nigeria inatumika tu kutoa pesa."

Wakati wa kutangaza mpango huo, CBN ilisema noti mpya zitaanza kutumika kuanzia Disemba 15 na zile za zamani zitaondolewa mwishoni mwa Januari.

Baadaye benki iliongeza muda hadi Ijumaa iliyopita. Lakini Mahakama ya Juu iliingilia kati na kusitisha tarehe hiyo ya mwisho lakini foleni nje ya benki zimendelea kuongezeka.

"Njia pekee ya uamuzi kutafanya kazi ni kuachilia noti za zamani kwenye mfumo ili kukabiliana na uhaba [lakini] kufanya hivyo kutaturudisha nyuma," anasema mwanauchumi Bw Alaje.

Madai ya kuhodhi

Matawi ya benki binafsi yamekuwa yakituhumiwa kwa kuhodhi noti hizo mpya.

Kwanza, bado walikuwa wakitoa noti za zamani badala ya mpya, hadi wiki ya tarehe ya mwisho, na hivyo kuziweka katika mzunguko.

Pili, mawakala wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Udanganyifu nchini, Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha, walivamia baadhi ya matawi ya benki na kuwakamata mameneja waliokuwa wakituhumiwa kuhodhi noti hizo mpya kwenye vyumba vya kuhifadhia fedha badala ya kuziweka kwenye mashine na kuwapa wateja.

"Benki hazifanyi kazi nzuri ya kusambaza fedha hizo. Mameneja wa benki wamekuwa wakiweka kando fedha nyingi kwa ajili ya watu wenye uhusiano na matajiri, wakitumia vibaya sera ya benki kuu," Dk Makinde anasema.

Kutokana na hayo, ukosefu wa noti mpya za naira umewakumba wale ambao kimsingi wanashughulika na pesa taslimu siku hadi siku, kama vile wauzaji sokoni na wachuuzi.

Iya Ruka, 52, anauza ndizi katika soko la Ojodu Berger, Lagos. Amelazimika kukubali malipo kupitia uhamisho wa benki - lakini hii haijamsaidia anapohitaji pesa.

"Wateja wangu wote wanasema hawana fedha, watalipa kupitia benki zao moja kwa moja, lakini nikienda benki hakuna fedha. Kwa hiyo nifanye nini?"

Kingsley, ambaye alitoa jina lake la kwanza tu, anauza vifaa vya simu ya rununu.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 27 aliniambia kuwa hajauza chochote katika siku chache zilizopita.

"Watu hulipa tu [kwa] uhamisho wa benki. Nikitaka kwenda nyumbani, lazima nienda Kituo cha Uuzaji (POS) ili kupata pesa na wanatoza pesa nyingi sasa."

Wachuuzi wa POS ni watu binafsi wanaosimama kando ya barabara mashine ya kadi ili kuwasaidia watu kuhamisha fedha ya kupata duma lakini ada yao iko ju sana.

'Mambo yatakuwa mazuri'

Mchuuzi mmoja, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alitetea hitaji la kutoza ziada.

"Nilipanga foleni kwa siku nzima katika benki ili kupata noti mpya na noti za zamani.

Ndiyo maana lazima walipe, kwa sababu tunapanga foleni," anasema kijana huyo wa miaka 25, ambaye anaendesha kioski huko Lekki.

Anaongeza kuwa hana uhakika ataendelea na biashara hiyo kwa muda gani, kwani benki hazina pesa.

"Baadhi ya wateja wanakukasirika na hata kukaribia kuzua vurugu - mimi huepuka kuwatazama. Wanasahau kuwa ninateseka pia, hali ilivyo sasa, inabidi nisafiri kwa saa moja kwenda nyumbani, na nimekuwa nikila tu garri [mihogo] ."

Chanzo: BBC