Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nigeria yahaha kuzima digrii za wiki sita

Degree Pic Wahitimu UDSM Nigeria yahaha kuzima digrii za wiki sita

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwandishi wa habari za uchunguzi wa Nigeria ameitoa usingizini Serikali yake kuhusu vyuo vikuu vinavyotoa masomo ya shahada (digrii) kwa wiki sita, badala ya miaka minne.

Kufuatia uchunguzi huo, Serikali ya Nigeria imetangaza kusimamisha tathmini na uidhinishaji wa shahada zote kutoka nchi jirani za Benin na Togo, huku ikisisitiza itapiga marufuku hata shahada za kutoka Kenya na Uganda kama zitakuwa za mtindo huo.

Pia, Serikali ya Nigeria imevipiga marufuku vyuo vikuu 18 vya kigeni vinavyofanya kazi nchini Nigeria na kuvitaja kama "viwanda vya kufyatua shahada,'' ikiwaonya Wanigeria kuepuka kujisajiri katika taasisi hizo.

Agizo hilo liliathiri vyuo vikuu vitano kutoka Marekani, sita vya Uingereza na vyuo vitatu vya elimu ya juu vya Ghana.

Shahada ya wiki sita

 “Unaletewa shahada yako, kama vile unavyoletewa pizza,” ni kauli ya mwandishi wa habari za uchunguzi wa Nigeria, Umar Audu.

Umar Audu, amefichua jinsi cheti chake cha shahada kutoka chuo kikuu chenye makao yake makuu mjini Cotonou nchini Benin, kwamba kilikabidhiwa kwake kama unavyoletwa pizza baada ya kukamilisha malipo.

Pia, Umar Audu amefichua kundi linaloshamiri la ulaghai wa vyeti vya vyuo vikuu katika nchi za Benin na Togo, ambalo lina utaalamu wa kuuza shahada za chuo kikuu kwa wanunuzi walio tayari nchini Nigeria.

“Hiki cheti kitaletwa kwako kama ulivyoagiza pizza au kitu fulani na unawapa eneo lako na unaletewa. Hilo ndilo lililonisukuma kufanya uchunguzi huu,” amesema Audu.

Habari hiyo ya uchunguzi iliyopongezwa na Serikali ya Nigeria na kufikia uamuzi wa kuvipiga marufuku baadhi ya vyuo vya kigeni nchini humo ilichapishwa Desemba 30, 2023 kwenye gazeti la Daily Nigerian.

Uamuzi wa Serikali Wizara ya Elimu ya Nigeria ilitoa taarifa ikishutumu vitendo vya baadhi ya Wanigeria kujihusisha na udanganyifu huo wa kupata shahada kwa njia ya mkato.

Kulingana na taarifa ya Augustina Obilor-Duru kwa niaba ya Mkurugenzi wa Vyombo vya Habari na Mahusiano ya Umma, Wizara ya Elimu ya Nigeria, uamuzi wa Serikali wa kusimamisha tathmini na uidhinishaji wa vyeti vya shahada kutoka nchi za Benin na Togo utaendelea kusubiri matokeo ya uchunguzi.

"Wizara ya Elimu inalaani vikali vitendo hivyo na kuanzia Januari 2, 2024 inasitisha tathmini na ithibati ya vyeti vya shahada kutoka Benin na Togo kusubiri matokeo ya uchunguzi ambao utahusisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria.

 “Kwa hiyo wizara inapenda kutoa wito kwa wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo, kuonyesha uelewa na kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kamati katika kutafuta suluhisho la kudumu ili kuzuia changamoto hiyo.”

"Wizara pia imeanza michakato ya kiutawala ya ndani ili kubaini iwapo baadhi ya maofisa wake kama wanahusika na mchezo huo mchafu.''

Mwaka 2020 aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Vyuo Vikuu, Profesa Abubakar Rasheed aliwahi kusema baadhi ya Wanigeria walikuwa wakinunua shahada bandia kutoka kwa kwenye vyuo vya ndani na nje ya Nigeria.

Pia, Septemba 2023, gazeti moja nchini Nigeria lilifichua namna ya chuo kimoja inavyouza shahada feki za heshima kwa Wanigeria.

Akizungumzia maendeleo hayo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu katika Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Teknolojia, Minna, Profesa Gbolahan Bolarin, alitoa wito wa kuanzishwa kwa bodi ya kuidhinisha shahada za vyuo vya kigeni nchini Nigeria.

 “Nadhani jitihada za kutafuta njia ya haraka ya kupata shahada ndiyo sababu kuu ya hili. Wanigeria, hasa vijana, wanakosa subira na wangetafuta njia zote za kukata kona.

"Zaidi ya kupiga marufuku shahada kutoka Togo na Benin, tunahitaji kuanzisha bodi ya uidhinishaji wa shahada za kigeni," alisema Profesa Bolarin.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live