Mkuu wa Majeshi ya Nigeria, Christopher Musa, ametangaza nia ya nchi hiyo ya kuongeza mapambano dhidi ya magaidi, majambazi na wahalifu wengine katika jitihada za kuimarisha utulivu ndani ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika yenye watu wengi zaidi barani humo.
Akizungumza katika mkutano wa masuala ya ulinzi uliofanyika Ijumaa huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria, Meja Jenerali Christopher Musa amesema, wanajeshi walioko chini ya amri yake wataenda kila upande kuhakikisha Nigeria na watu wake wanaishi salama.
Amesema: "Ninamhakikishia kila Mnigeria kwamba utafika wakati atajisikia yuko salama kwani vikosi vya jeshi vinafanya kazi ya kuwalinda na kuwatumikia."
Mkuu huyo wa majeshi ya Nigeria pia ameahidi kulipa umuhimu suala la ustawi wa wanajeshi akisema: "askari aliyeshiba na kutunzwa vizuri hutoa huduma bora kadiri awezavyo."
Magaidi wa Boko Haram Wakati huo huo watu watatu wenye silaha wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi kwenye Jimbo la Delta la kusini mwa Nigeria.
Taarifa ya Jeshi la Polisi la Nigeria imesema kuwa, mapigano baina ya jeshi hilo na kundi la majambazi yalizuka baada ya majambazi hao waliokuwa na silaha kuwatishia wasafiri kwenye barabara ya mji wa Warri .
Taarifa hiyo imetolewa na Bright Edafe, msemaji wa polisi katika jimbo la Delta na kuongeza kuwa, baada ya kupata taarifa hiyo, timu ya polisi ilitumwa mara moja kwenye eneo hilo kwa ajili ya kuwatimua majambazi hao wenye silaha.
Amesema: "Maafisa wa polisi waliwashambulia kwa bunduki majambazi hao na kuwajeruhi vibaya watatu kati yao na majambazi wengine wa genge hilo walitoroka na majeraha ya risasi."
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi, zoezi la kuwasaka majambazi hao waliotoroka wakiwa na silaha lingali linaendelea.