Shambulio la ndege zisizo na rubani la jeshi la Nigeria liliwaua kwa bahati mbaya raia 85 juzi Jumapili katika kijiji kimoja kaskazini-magharibi mwa Jimbo la Kaduna huko Nigeria.
Rais Bola Tinubu wa Nigeria leo ameagiza kufanyika uchunguzi baada ya jeshi la nchi hiyo kukiri kuwa moja ya ndege zake zisizo na rubani (droni) zimeshambulia kwa bahati mbaya kijiji cha Tudun Biri wakati wenyeji wa kijiji hicho walikuwa wakisherehekea tamasha la Kiislamu.
Jeshi la Nigeria halijatangaza idadi ya watu waliouliwa katika shambulio hilo la droni lakini wakazi wa kijiji hicho wamesema kuwa watu 85 wameuawa wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.
Wakati huo huo Ofisi ya Kanda ya Kaskazini magharibi huko Nigeria imepokea taarifa kutoka kwa maafisa wa eneo ikieleza kuwa miili 85 ya raia tayari imezikwa. Wakala wa Taifa wa Usimamizi wa Dharura Nigeria (NEMA) umeripoti kuwa watu wengine 66 wanapatiwa matibabu hospitalini kufuatia shambulio la droni la jeshi la Nigeria juzi Jumapili katika kijiji cha Tudun Biri.
Vikosi vya kijeshi vya Nigeria vimeeleza kuwa mara nyingi hutekeleza mashambulizi ya anga katika mapambano dhidi ya wanamgambo wahalifu huko kaskazini magharibi na kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi la Nigeria
Rais Tinubu amelitaja tukio hilo kuwa la kusikitisha sana na lenye kuumiza akionyesha huzuni kufuatia kuuliwa raia hao katika shambulio la jeshi.