Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Niger yavunja ushirikiano wa kijeshi na Marekani

Niger Na Umoja Wa Ulaya Niger yavunja ushirikiano wa kijeshi na Marekani

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Niger imetangaza kwamba "bila kupoteza muda" inavunja makubaliano yake ya ushirikiano wa kijeshi na Marekani.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa kijeshi wa Niger imesema, serikali hiyo imeamua "kuyalaani bila kupoteza muda" makubaliano yanayohusisha wanajeshi wa Marekani na wafanyakazi wa kiraia wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon walioko ndani ya Niger.

Taarifa hiyo ilisomwa jana ioni kwenye televisheni ya taifa ya Niger na msemaji wa utawala wa kijeshi Kanali Amadou Abdramane.

Uamuzi huo umechukuliwa siku chache baada ya ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani, uliojumuisha Mkuu wa Kamandi ya nchi hiyo barani Afrika, Jenerali Michael Langley, kukamilisha ziara yake ya siku tatu katika taifa hilo la Afrika.

Ujumbe wa Pentagon ulikutana na maafisa wakuu kadhaa wa Niger, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Ali Mahaman Lamime Zeine katika hatua iliyolenga kushawishi kuendelezwa makubaliano hayo, lakini haukufanikiwa kukutana na kiongozi wa nchi hiyo, Jenerali Abdourahamane Tchiani.

Jenerali Abdourahamane Tchiani Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, Niger imesikitishwa na nia iliyoonyeshwa na ujumbe wa Marekani ya kuwanyima watu huru wa Niger haki ya kuchagua washirika wao na aina ya ushirikiano wenye uwezo wa kuwasaidia kikwelikweli kupambana na ugaidi, na akaongeza kuwa Wamarekani hawakufuata itifaki ya kidiplomasia walipoelekea Niger na hata hawakuwafahamisha wenyeji wao kuhusu ajenda ya mazungumzo na tarehe ya kuwasili kwao.

Marekani ingali imeweka wanajeshi wake1,000 nchini Niger kwenye kituo cha ndege zisizo na rubani kilichojengwa kwa gharama ya dola milioni 100.

Shughuli za Pentagon katika kituo hicho zimekuwa chache tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Niger Julai 2023 huku Washington imezuia misaada yake kwa serikali ya kijeshi ya nchi hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alifanya ziara ya nadra nchini Niger mwaka mmoja uliopita kwa matumaini ya kutoa msukumo kwa rais Mohamed Bazoum, mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi katika kampeni ya kinachoitwa juhudi za kiusalama za kupambana na watu wenye itikadi na misimamo mikali.

Miezi minne tu baada ya ziara hiyo ya Blinken, jeshi lilimwondoa Bazoum madarakani na kumweka kwenye kizuizi cha nyumbani.

Baada ya kushika hatamu za uongozi wa nchi, watawala wa kijeshi nchini Niger walichukua msimamo mkali dhidi ya mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa, na kulazimisha kuondolewa wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwepo Niger kwa karibu muongo mmoja.

Huko nyuma, Jeshi la Niger lilifanya kazi kwa karibu na Marekani.

Lakini sasa limeonyesha hamu ya kuwa na ushirikiano na Russia, lakini bila ya kuwa na ukuruba kamili na Moscow kama ilivyo kwa majirani zake wa Mali na Burkina Faso zinazoongozwa pia na tawala za kijeshi.../

Chanzo: www.tanzaniaweb.live