Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Niger: Waandamanaji waapa kuvamia kituo cha kijeshi Ufaransa

Wananchi Kituo Niger Niger: Waandamanaji waapa kuvamia kituo cha kijeshi Ufaransa

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maelfu ya waandamanaji nchini Niger wamefanya maandamano karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu Niamey kwa lengo la kubainisha uungaji mkono wao kwa serikali ya kijeshi na kutaka wanajeshi wa Ufaransa waondoke mara moja katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waandamanaji hao walikusanyika karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa katika mji mkuu siku ya Jumapili, huku wakipeperusha bendera za Niger na kubeba mabango yenye kauli mbiu za kupinga Ufaransa.

"Hatutaki jeshi la Ufaransa nchini Niger," mwaandamanaji mmoja alisema, "Waache Wafaransa waondoke."

Mwandamaji mwingine alisikika akisema: "Wafaransa wanasema kuwa Niger ni nchi maskini, lakini tunapowaambia warudi nyumbani, wanakataa."

Waandamanaji hao pia wamepiga nara dhidi ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS ambayo imeiwekea Niger vikwazo vya kiuchumi na kutishia kuchukua hatua za kijeshi kumrejesha madarakani rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum.

Waandamanaji hao wametishia kuvamia kambi ya jeshi la Ufaransa ikiwa wanajeshi hao hawataondoka nchini humo ndani ya wiki moja.

Pia wametoa wito wa kutimuliwa balozi wa Ufaransa, Sylvain Itte, baada ya mwanadiplomasia huyo kupewa makataa ya saa 48 kuondoka nchini humo.

Siku ya Ijumaa, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo alitangaza kuwa balozi wa Ufaransa ana saa 48 kuondoka, akisema amekataa kukutana na viongozi wapya wa kijeshi mbali na hatua za serikali ya Ufaransa ambazo "ni kinyume na maslahi ya Niger."

Majenerali wa jeshi la Niger walimpindua Rais mshirika wa Ufaransa, Mohamed Bazoum Julai 26. Tangu wakati huo Waniger wameishutumu Ufaransa kwa kutaka kuingilia kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ili kumrejesha madarakani Bazoum.

Jeshi limechukua madaraka nchini Niger huku kukiwa na wimbi kubwa la chuki dhidi ya Wafaransa, ambapo watu wa Niger wanaishutumu nchi hiyo ya Ulaya kwa kuingilia masuala yao ya ndani.

Tangu kuchukua mamlaka, Waniger mara kadhaa wamejitokeza kwa nguvu kuonyesha uungaji mkono wao kwa viongozi wa kijeshi na kupinga tawala za zamani ambazo wamezitaja kuwa vibaraka wa Magharibi.

Mapema mwezi huu, maelfu ya waandamanaji dhidi ya Magharibi waliingia barabarani kupinga mipango ya mataifa ya Afrika Magharibi kupeleka kikosi cha kijeshi nchini humo.

Ufaransa ilikuwa utawala wa kikoloni katika Afrika Magharibi hadi 1960. Tangu uhuru, nchi hiyo ya Ulaya imedumisha uhusiano wa kibiashara na uwepo wa kijeshi katika eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live