Watu wameanza kukusanyika katika uwanja mmoja katikati mwa Niamey, mji mkuu wa Niger, kuonyesha uungaji mkono wao kwa mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita.
Katika maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo, muungano wa asasi za kiraia ulitoa wito kwa watu kujitokeza kukemea vikwazo vilivyowekwa na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS.
ECOWAS Inasema ikiwa rais Mohamed Bazoum hatarejeshwa inaweza kutumia nguvu.
Karibu wote wanaokusanyika katika uwanja wa uhuru katika siku ya uhuru kwa ajili ya kuonyesha uungaji mkono wao ni vijana huku wakiwa na kauli mbiu za Ufaransa na bendera chache za Urusi.
Licha ya kuonyesha uungaji mkono kwa watu waliompindua rais, wengi nchini Niger wanapinga mapinduzi hayo.
Kuna mtazamo kwamba ilikuwa ni hatua ya wanajeshi waandamizi ambao walikuwa katika hatari ya kubadilishwa na kupoteza madaraka yao.
Lakini sasa wakati wanatafuta kuhalalisha hatua yao, hisia za kupinga Ufaransa zinasikika.
Matukio haya ni sawa na yale yaliyofanyika katika nchi za Mali na Burkina Faso ambapo viongozi wa mapinduzi wameimarisha uhusiano na Urusi.