Mahakama nchini Niger imeamuru mgodi wa madini ya uranium unaomilikiwa na kampuni ya Canada kaskazini mwa nchi hiyo kusitisha shughuli zake baada ya wanamazingira kuwasilisha kesi mahakamani, chanzo cha mahakama kimeliambia shirika la habari la AFP Jumanne.
Mahakama mjini Agadez, katika uamuzi ilioutoa Jumatatu, iliamuru kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji madini za kampuni ya SOMIDA, ambayo kwa kiasi kikubwa inamilikiwa na kampuni ya Canada ya Global Atomic , ambayo kiishara, ilianza uchimbaji wa madini katika eneo lililo karibu mwezi Novemba mwaka jana.
Muungano wa mashirika ya kiraia mwezi Januari mwaka huu, uliomba Mahakama kuruhusu kuendeshwa tafiti mpya kuhusu athari za mazingira ukidai kuwa tafiti za awali hazikuwa sahihi na zilifanywa bila kushauriana vya kutosha na wakazi.
Niger ni moja ya vyanzo vikuu vya uranium duniani, madini ambayo yanatafutwa na mataifa duniani kote kama chanzo cha nishati ya nyuklia ambayo inaweza kupunguza kutegemea nishati ya mafuta.
Lakini hofu ya usalama na wasiwasi wa kimazingira juu ya utupaji wa taka zenye sumu ya nyuklia bado zipo, ikimaanisha kuwa nchi hiyo maskini ya Sahel isiyo na bahari bado haijanufaika vya kutosha na uchimbaji wa madini hayo.
Global Atomic inamiliki asilimia 80 ya mtaji katika kampuni ya SOMIDA, huku serikali ya Niger ikimiliki asilimia 20.