Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni wakati gani ambapo Jeshi huingilia usalama wa ndani Kenya?

Marekani Yawahamisha Wafanyakazi Wa Ubalozi Haiti Huku Kukiwa Na Vurugu Za Magenge Ni wakati gani ambapo Jeshi huingilia usalama wa ndani Kenya?

Tue, 16 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kufuatia maandamano ya Gen Z yaliomshinikiza rais william Ruto kuutupilia mbali muswada wa fedha wa 2024, serikali ililazimika kuomba msaada wa jeshi ili kuwasaidia maafisa wa polisi waliozidiwa nguvu na waandamanaji kuleta utulivu kote nchini.

Licha ya baadhi ya vijana hao kupigwa risasi na wengine kuuawa, walifanikiwa kuingia katika majengo ya bunge ,ambapo wabunge walikuwa wakipitisha muswada huo wa fedha uliozua utata licha ya pingamizi kutoka kwa Wakenya wengi.

Kilichofuatia ilikuwa mguu niponye kwa viongozi hao waliokuwa wakihofia usalama wao, huku vijana hao wakiingia na kutekeleza uharibifu mkubwa katika jumba hilo la kutunga sheria , ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya taifa la Kenya.

Baadaye serikali ilitafuta msaada kutoka kwa jeshi ili kuwasaidia maafisa wa polisi licha ya Chama cha mawakili nchini LSK kuzua pingamizi mahakamani.

Bunge baadaye liliidhinisha hatua hiyo.

Mara ya mwisho kwa wanajeshi wa Kenya kuamrishwa kuweka usalama katika miji mikuu ya Kenya ni wakati wa jaribio la mapinduzi la mwaka 1982 ambapo waandalizi wake walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa huku mamia ya Wakenya wakipoteza maisha yao.

Je mahakama ilitoa uamuzi gani kuhusu jeshi? Akitoa uamuzi wake Jaji wa mahakama kuu alitoa idhini kwa serikali kutumia Jeshi ili kuweka usalama kufuatia maandamano hayo yaliojaa ghasia na kuwashinda nguvu maafisa wa polisi.

Uamuzi huo ulitokana na hatua ya waziri wa ulinzi Aden Duale kulitaka jeshi kusaidia maafisa wa polisi kuimarisha usalama.

Magari ya kijeshi baadaye yalionekana yakipiga doria katika barabara za Nairobi huku wanajeshi waliojihami wakiwasaidia maafisa wa polisi katika kuzuia wizi na uharibifu wa mali.

Cha kushangaza ni kwamba waandamanaji waliwakumbatia maafisa hao na kuwapongeza walipokuwa wakipiga doria zao, na hali ya utulivu iliporudi wanajeshi hao walirudi katika kambi zao wakiwaacha polisi kuendelea na kazi ya kuweka usalama.

Waandamanaji Kenya walipovamia bunge Je, ni wakati gani ambapo jeshi huingilia usalama wa ndani wa nchi? Kulingana na waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya Kithure Kindiki , uwekaji wa wanajeshi ndani ya nchi kuimarisha usalama umeelezewa kwa kina katika Ibara ya 241 ya Katiba.

Kindiki ambaye alikuwa akihojiwa na runinga ya The Citizen nchini Kenya anasema kwamba jeshi huombwa kusaidia tu iwapo kuna ‘tishio la dharura.’

Kulingana na waziri huyo tishio la dharura nchini Kenya linaweza kuelezewa kuwa tishio la usalama linalojitokeza na kusababisha mkazo mkubwa unaohitaji usaidizi ama operesheni maalum.

‘’Ni lazima iwe hali ambayo haijapangwa ambayo ni tishio kwa usalama wa taifa ambapo operesheni maalum pamoja na usaidizi unahitajika’’, alisema bwana Kindiki akinukuliwa na runinga ya Citizen Kenya.

Lakini ni nani haswa anayeamua kuna tishio la Usalama nchini? Kulingana na waziri Kindiki ambaye pia ni wakili wa masuala ya kikatiba uamuzi wa kile kinachojumuisha dharura ya usalama ni uamuzi unaofanywa na vyombo vya usalama wa kitaifa vilivyoanzishwa chini ya kifungu cha 239 hadi 240 cha katiba.

Kwa mujibu wa Kindiki, wakati kuna tishio kama hilo, waziri wa masuala ya mambo ya ndani kwa kushauriana na makamanda wa idara ya maafisa wa polisi huwasilisha ombi kwa Wizara ya ulinzi kwa kutumia kifungu cha 241 3b au 3c ya katiba.

Kindiki anasema kwamba waziri hutumia utaratibu kupitia mashauriano na jeshi la KDF na mara uamuzi unapotolewa inspekta jenerali wa polisi na Mkuu wa kikosi cha ulinzi hukutana kupanga kile kinachoitwa agizo la operesheni.

Mara tu baada ya waziri kutangaza suala hilo kwenye gazeti la serikali, agizo la utendakazi linakubaliwa kati ya inspekta jenerali wa huduma ya kitaifa ya polisi na jeshi, alihitimisha bwana Kindiki.

Je, wanajeshi hupewa majukumu gani? Kulingana na kifungu cha 35 cha Sheria ya jeshi la KDF katika katiba ya Kenya, wakati wowote ambapo Jeshi la Ulinzi au sehemu yoyote au mwanachama wake ametumwa kuwasaidia maafisa wa polisi katika operesheni ya usalama, mwanajeshi wa KDF atakuwa na mamlaka sawa na kutekeleza majukumu sawa na yale aliyopewa afisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi.

Mamlaka na majukumu yanaweza tu kutekelezwa kwa ufanisi kwa udumishaji wa sheria na utaratibu wa kuhifadhi usalama wa ndani wa Nchi.

Hatahivyo, mamlaka hayo hayatajumuisha wajibu wa kuchunguza uhalifu.

Sheria inaeleza kuwa katika operesheni hiyo au msaada huo wa polisi, askari wa Jeshi la Ulinzi anayemkamata au kumweka kizuizini mtu yeyote au kukamata kitu au kitu chochote atalazimika haraka iwezekanavyo kukabidhi kitu hicho ama mtu huyo kwa polisi. Athari za kupatia jeshi jukumu la kuimarisha usalama ndani ya nchi

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisasa nchini Kenya David Burare, rais anapolitumia jeshi ni kwa manufaa yake kwasababu linaweza kwa urahisi kuleta udhabiti ndani ya taifa hususan wakati ambapo maafisa wa polisi wamezidiwa.

Hatahivyo ameonya kwamba ni maamuzi hatari kutumia jeshi kuweka usalama ndani ya nchi kwasababu maafisa hao hawana mafunzo ya kudhibiti makundi ya watu hivyobasi wanaweza kusababisha maafa zaidi ya ilivyotarajiwa.

‘Iwapo wanakabiliana na waandamanaji waliojawa na ghadhabu, kwa mfano je, watatumia vifaa gani kuwadhibiti ilihali hawana vitoa machozi wala yale maji ya kuwasha?’’, aliuliza bwana Burare.

Bwana Burare anaongezea kwamba wanajeshi vile vile wanaweza kuchukua fursa ya hali mbaya ya kiusalama na kuunga mkono vuguvugu la maandamano dhidi ya serikali iliopo.

‘Ni hali ambayo imetokea katika mataifa mengi ya Afrika’, alisema mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa.

Anasema kiuchumi taifa linalokuwa na wanajeshi barabarani kuweka usalama huonesha ishara za kutokuwa na udhabiti hali inayowafukuza wawekezaji mbali na watalii .

Chanzo: www.tanzaniaweb.live