Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni mwanzo wa mwisho wa uongozi wa wazee Afrika?

Wazee Mksz Ni mwanzo wa mwisho wa uongozi wa wazee Afrika?

Wed, 22 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Kama kipimo cha ujana ni chini ya umri wa miaka 50, basi Afrika ilikombolewa na vijana. Ukianzia kwa Kwame Nkrumah, aliyeiwezesha Ghana kupata uhuru akiwa na umri wa miaka 47, hadi Mwalimu Julius Nyerere, aliyeiondoa Tanganyika kutoka kwa wakoloni Uingereza, akiwa na umri wa miaka 39.

Ahmed Sekou Toure, aliyeipa Guinea uhuru, akiwa na umri wa miaka 36, halafu Kenneth Kaunda, aliyewang’oa Waingereza Zambia, alipokuwa na umri wa miaka 40. Kisha, Ahmadou Ahidjo, ambaye aliiwezesha Cameroon kuwa huru, umri wake ukisoma miaka 35.

Gambia, Dawda Jawara, aliiwezesha nchi hiyo kuwa taifa huru alipokuwa na umri wa miaka 40. Patrice Lumumba, alifanikisha kuifanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuwa nchi huru, siku mbili kabla hajatimiza umri wa miaka 35. Yupo Seretse Khama, aliyeipa Botswana uhuru akiwa na umri wa miaka 44.

Ni muhtasari, kuonyesha asili ya uhuru wa Afrika. Zipo nchi nyingi tu ambazo uhuru wake uliwezeshwa na watu wa makamo mpaka wazee. Hata hivyo, lengo ni kudhihirisha kuwa Afrika ilipokuwa inajichomoa kwenye makucha ya wakoloni, vijana ndiyo walikuwa mstari wa mbele.

Mei 10, 2024, Mahamat Deby, akiwa na umri wa miaka 40, alikula kiapo kuiongoza Chad. Deby, alishinda Uchaguzi wa Urais Chad, uliofanyika Mei 6, 2024. Awali, Deby, alianza kuiongoza Chad kijeshi akiwa na umri wa miaka 37, kufuatia kifo cha baba yake, Idriss Deby, aliyefia madarakani Aprili 20, 2021.

Mwezi mmoja kabla, Wasenegali waliushangaza ulimwengu, walipomchagua Basirou Faye, mwenye umri wa miaka 44, kuwa rais wa nchi yao. Haikuwa mara ya kwanza Senegal kuchagua rais kijana, kwani hata Rais wa Pili wa nchi hiyo, Abdou Diouf, aliingia ofisini mwaka 1981, alipokuwa na umri wa miaka 45.

Maajabu ya Faye, ni jinsi alivyochaguliwa kuwa rais katika zama za sasa, ambazo vijana wa zamani waliozeekea madarakani, hawataki kuachia madaraka. Halafu, wazee wanaopisha, wanakabidhi usukani kwa wazee wenzao, wakidai vijana hawajakomaa. Wakati vijana ndiyo walioipa uhuru Afrika kwa sehemu kubwa.

Chanzo: Mwananchi