Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngoma bado mbichi! Ruto, Raila warushiana shutuma za rushwa

Raila Odinga Ruto.jpeg Ruto, Raila warushiana shutuma za rushwa

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amesema kampeni za mpinzani wake katika mbio za urais, Raila Odinga, zinafadhiliwa kupitia fedha za mapambano dhidi ya Uviko-19 ambazo ni mali ya umma.

Ruto amesema, fedha za msaada zilizoingizwa Kenya kwa ajili ya Uviko-19, zimegeuzwa matumizi na sasa ndizo zinatumika kufanikisha kampeni za Raila kusaka madaraka.

Tangu kampeni zianze, Raila ndiye amekuwa akiwaambia Wakenya kujitenga na Ruto pamoja na mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua, kwa sababu si watu waaminifu na ni wezi. Ruto, anayegombea urais kupitia chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa ushirika wa vyama uliopewa jina la Kenya Kwanza, alisema kwa sasa Raila sio mtu wa kuwafundisha kuhusu rushwa kwa sababu ni mnufaika wa ufisadi wa mali za umma.

Bila kufafanua jinsi Raila anavyonufaika na fedha za umma, Ruto alisema kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani anayegombea urais kwa leseni ya Azimio la Umoja One Kenya, amepata ufadhili wa fedha za Uviko-19.

“Unatupa darasa la kupambana na rushwa wakati wewe mwenyewe ni mnufaika wa fedha za umma,” alisema Ruto kwenye mkutano wa hadhara, Kaunti ya Kiambu.

Hata hivyo, Ruto hakusema kuwa Raila amechota fedha za Uviko-19, bali alieleza kwamba mabilionea waliotajirika kupitia fedha za janga hilo, ndio ambao wanafadhili kampeni za Raila.

Nchini Kenya, kumekuwa na kashfa kubwa ya uchotaji wa fedha za Kenya, Sh7.8 bilioni, ambazo ni Sh156 bilioni kwa sarafu ya Tanzania. Kampuni ya Shadowy na nyingine zinadaiwa kupata fedha hizo kwa kudanganya bei za barakoa na vifaa vya kupambana na Uviko-19.

Inabainishwa kwamba wachotaji hao wa fedha za umma, wamenufaika kupitia fedha za Uviko-19 kwa kushirikiana na maofisa wasio waaminifu wa Mamlaka ya Ugavi wa Dawa Kenya (Kemsa). Ruto hajataja ni akina nani walionufaika na fedha za Uviko-19 wanaomfadhili Raila, ila kwenye mikutano yake kwenye Kaunti ya Kiambu, alisisitiza kuwa kampeni zote za Azimio la Umoja ni kwa msaada wa wachotaji wa fedha za janga la Uviko-19.

Kuhusu mapambano ya rushwa, Ruto aliahidi kuwa akishinda urais, atawezesha taasisi za kupambana na rushwa zifanye kazi kwa uhuru pasipo kuziingilia, akidai hiyo itakuwa njia muhimu ya kutokomeza ufisadi.

Aliahidi pia kufanikisha kutungwa kwa sheria mpya ambazo zitatumika ipasavyo kukabiliana na rushwa na kuondoa mianya ya sasa ambayo inawafanya watu wengi kuendelea kupora mali za umma.

Ahadi nyingine ya Ruto aliyoitoa akiwa Kaunti ya Kiambu ni kuupa ruzuku Mfuko wa Bima ya Taifa (NHIF), Kenya, ili kuwapunguzia mzigo wa michango ya mwezi, kutoka Sh500 ya Kenya (Sh10,000), mpaka Sh300 (Sh6,000).

Ruto aliahidi kuwa familia maskini na wenye kuishi katika mazingira magumu, watapata matibabu bure mara atakaposhinda na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Ni majibu ya Raila

Kambi ya Azimio la Umoja imekuwa ikirusha mashambulizi kwa Ruto kwamba kiongozi huyo ni kinara wa kupora mali za umma na kujitajirisha binafsi na watu waliomzunguka.

Ruto alipomtangaza Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza wake, Raila alisema: “Mnaona aina ya mtu ambaye anataka awe Naibu Rais? Ni mwizi. Hatutakubali wezi wawili wakamate madaraka ya juu nchini.”

Gachagua ni mdogo wa aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Nyeri, Nderitu Gachagua, aliyefariki dunia mwaka 2017 kwa maradhi ya saratani ya kongosho.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Gachagua aliajiriwa Ofisi ya Rais kama Ofisa Kada wa Wilaya, akishughulika na Wilaya ya Kakamega. Kisha alikuwa msaidizi wa waziri wa masuala ya umma mwaka 1991.

Mwaka 1997 mpaka 1999, Gachagua alikuwa Ofisa Mkuu wa Wilaya ya Laikipia, Ng’arua. Gachagua alishakuwa msaidizi binafsi wa Rais Uhuru Kenyatta. Kuhusu kashfa, Gachagua amewahi kutuhumiwa kuingilia ofisi ya Gavana wa Nyeri, kipindi kaka yake anaumwa kisha akawa anafanya kazi kama kaimu gavana wakati Naibu Gavana alikuwepo.

Mamlaka ya Uokoaji wa Mali za Umma Kenya (ARA), imewahi kumtuhumu Gachagua kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu ambapo, kesi hiyo bado ipo mahakamani.

ARA wanamtuhumu Gachagua kupokea fedha, Shilingi za Kenya 12.5 bilioni (Sh250 bilioni) kupitia akaunti zake tatu kwenye Benki ya Rafiki Micro Finance. Gachagua alikanusha kuhusika na utakatishaji huo.

Kiasili, Gachagua ametokea kwenye familia ya kawaida. Maisha ya mwanzoni alikuwa mtumishi wa umma, ingawa ghafla aliibuka bilionea na mwanasiasa.

Alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 2017. Utajiri mkubwa alionao ndio unasababisha aonekane ni mtu aliyepata mali kwa njia haramu.

Simulizi ya utajiri wa Gachagua haitofautiani sana na ile ya Ruto, ambaye naye ametokea koo maskini, lakini kipindi cha uongozi wa Rais Daniel Moi, alitumia fursa kujitajirisha binafsi na sasa ni tajiri mkubwa Kenya.

Simulizi kuhusu Ruto kutajirika kwa ufisadi ni za muda mrefu. Hata akiwa Naibu Rais, amekuwa akishutumiwa kujilimbikizia mali nyingi kinyume na Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma Kenya.

Hata hivyo, Raila naye amekuwa akipopolewa mawe kwamba nyakati za mwisho za uongozi wa Rais Moi, alijiweka karibu yake na kufanikiwa kutengeneza mrija mrefu wenye kuchota mali za umma.

Na hiyo ndio sababu, wakati Raila na mgombea mwenza wake, Martha Karua pamoja na kambi yote ya Azimio la Umoja, wakiwapopoa mawe Ruto na Gachagua, nao pia wanapata ujasiri wa kujibu na kurudisha mapigo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live