Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngano kutoka Ukraine kupunguza njaa Kenya-Wachumi

Ngano Kutoka Ukraine Kupunguza Njaa Kenya Wachumi Ngano kutoka Ukraine kupunguza njaa Kenya-Wachumi

Fri, 24 Mar 2023 Chanzo: Voa

Wachumi wa Kenya wanasema ngano iliyoagizwa hivi karibuni kutoka Ukraine inaweza kusaidia kupunguza njaa katika maeneo yenye ukame na kupunguza bei ya juu ya vyakula.

Tani elfu thelathini za ngano ziliwasili Kenya Jumatatu chini ya Mpango wa Nafaka wa Black Sea unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambapo Russia ilikubali kutozuia usafirishaji wa nafaka wa Ukraine. Lakini Rais wa Russia Vladimir Putin alionya wiki hii kwamba Moscow inaweza kuachana na mpango huo ndani ya siku 60.

Kuongezeka kwa gharama ya bidhaa za nafaka kama vile ngano kumewaacha waokaji mikate kama Harrison Kiai katika mtego wa bei ya juu ya unga wa ngano. Kiai anasema siku hizi faida yake ni ndogo sana "bei za vitu vya kuoka kama unga, sukari, ukilinganisha na za mwisho labda miaka miwili, gharama ilikuwa kidogo kwa hiyo changamoto tunazo sasa hivi za kuongeza gharama, ambazo labda mteja hana raha nazo kwa sababu unapoenda sokoni mambo yamepanda juu" alisema Kiai.

Harrison anaamini kwamba uagizaji wa ngano hivi karibuni kutoka Ukraine utasaidia kupunguza kupanda kwa bei ya unga. Tani elfu thelathini za ngano kutoka Ukraine ziliwasili Kenya wiki hii.

Shehena hiyo ambayo ni sehemu ya mpango wa kibinadamu wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy wa nafaka kutoka Ukraine ilisafirishwa chini ya Mpango wa Nafaka wa Black Sea unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Andriy Pravednky ni balozi wa Ukraine nchini Kenya anasema "ahadi yetu ya usalama wa chakula ni kwa hakika meli inakuja na sio meli ya kwanza kuja Afrika na hata ya pili na tunapanga meli zaidi kuja mwishoni mwa mwaka huu kufikisha tani milioni 5 za nafaka kwa nchi za Kiafrika pekee. Lakini tunapaswa kutambua kwamba kutokana na uvamizi wa Russia mazao nchini Ukraine yalishuka."

Uzalishaji wa kilimo na mauzo ya nje ya Ukraine ulivurugwa sana na uvamizi wa Russia na nchi nyingi za Kiafrika ambazo zinategemea sana nafaka na ngano za Ukraine zimepata taabu kutokana na uhaba wa bidhaa muhimu na bei ya juu ya chakula tangu wakati huo.

Mpango wa Nafaka wa Black Sea uliokubaliwa mwaka jana unakusudiwa kuruhusu uuzaji wa vyakula vya Ukraine kufikia masoko ya nje. Walakini Rais wa Russia Vladimir Putin alionya wiki hii kwamba nchi yake inaweza kujiondoa kutoka kwenye makubaliano hayo la sivyo usafirishaji wa bidhaa zake za kilimo uwezeshwe.

Kabla ya uvamizi huo Kenya iliagiza tani milioni 2.4 za ngano kutoka Ukraine kila mwaka.

Ingawa nafaka iliyowasili nchini Kenya inaweza kusaidia kupunguza njaa katika maeneo yaliyokumbwa na ukame wanauchumi wanasema serikali za Afrika lazima zitengeneze njia za kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje kama vile kuongeza uzalishaji wa ndani.

Bila hivyo anasema mchumi Silas Omenda nchi kama Kenya zitakaa kutegemea huruma za nje "Tunaweza kufanya mambo haya mengine yote lakini linapokuja suala la gharama zetu za nishati ambazo sasa ni kichocheo cha kuongeza thamani ni ndoto mbaya na pia utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje pia umetuweka kwenye athari mbaya za mfumuko wa bei kwenye soko la kimataifa kumaanisha kwamba hatuna udhibiti wa kile kinachotokea Ukraine na Russia.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani linasema kuvurugwa kwa usafirishaji wa chakula kutoka Ukraine na Russia kumewaacha takriban watu milioni 345 wakikabiliwa na uhaba wa chakula.

Chanzo: Voa