Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndoa za utotoni zatajwa changamoto Afrika

Ndoa Utotoniiiii.jpeg Ndoa za utotoni zatajwa changamoto Afrika

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tatizo la ndoa za utotoni linatajwa kuendelea kukabili mataifa mengi ya Afrika, huku ikielezwa kuchangia kuchangia kuwa chanzo cha kukosekana kwa haki za binadamu kwa watoto wa kike barani humo.

Kutokana na sababu hiyo, Kamisheni ya Afrika ya haki za binadamu na watu, imepanga kushirikiana na wadau wa masuala ya haki barani humo kusaidia watoto.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 9, 2023, na Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Kamishna Remy Lumbu, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha baada ya kumalizika kikao cha kawaida cha 77 cha kamisheni hiyo kilichoanza Oktoba 20, mwaka huu.

Amesema ni muhimu wadau wa masuala ya haki za binadamu kusaidia watoto barani Afrika kwani bado jamii nyingi zinaozesha watoto wakiwa katika umri mdogo.

"Tunaendelea kushirikiana na serikali na wadau wa masuala ya haki za binadamu Afrika,kwani ndoa za utotoni bado ni shida kubwa jamii nyingi zinaozesha watoto hivyo tuangalie namna gani tunaweza kusaidia watoto Afrika," amesema

Kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu barani humo, amesema kupitia kikao hicho cha siku 21 wamejadiliana masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kulinda na kutetea haki za binadamu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo kutoa elimu zaidi kwa wananchi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Janet Sallah Njie, amesema kikao hicho pamoja na masuala mengine wamejadiliana kuhusu ukeketaji kwa watoto wa kike ambapo kuna kamati maalum ya kushughulikia haki za watoto na kuzingatia Itifaki ya Maputo.

Naye Kamishna Hatem Essaiem,amesema ni muhimu nchi wanachama kuheshimu maazimio na maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCPHR), ili kulinda haki za binadamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live