Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi za EU zatakiwa kuondoa vikwazo Burundi

Cb12f7cccbab3e4b8a5fb1bb3d9a97ca.jpeg Nchi za EU zatakiwa kuondoa vikwazo Burundi

Tue, 15 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki ametoa wito kwa nchi wanachama za Umoja wa Ulaya (EU) kuondoa vikwazo dhidi ya Burundi kwani imefungua ukurasa mpya na iko tayari kusonga mbele.

Dk Mathuki amesema vikwazo hivyo vinawaumiza sio wananchi wa Burundi pekee, bali watu wote wa ukanda wa Afrika Mashariki.

“Natoa wito kwa EU kuwa tushirikiane kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wa Burundi,” alisema Dk Mathuki wakati akizungumza na ujumbe wa EU nchini Tanzania juu ya kuongeza misaada kutoka umoja huo katika mchakato wa mtangamano wa Afrika Mashariki.

Alisisitiza umuhimu wa EU kufanya kazi na EAC ili kuwezesha kufikia malengo yaliyo katika mchakato wa mtangamano wa jumuiya hiyo.

EU imeweka vikwazo dhidi ya Burundi tangu mwaka 2015 wakati wa migogoro ya ndani ya nchi hiyo baada ya aliyekuwa Rais wake Pierre Nkurunziza kutaka kuongeza muda wa utawala wake kwa muhula wa tatu.

Katika hafla hiyo hiyo, Katibu Mkuu wa EAC na timu yake walipata fursa kujadiliana na ujumbe wa EU kuhusu maeneo ya vipaumbele katika mtangamano huo yanayohitaji msaada kutoka Programu ya EU kwa mwaka 2021-2027.

Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuongeza fursa kwa sekta binafsi katika mtangamano wa EAC, kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa utawala wa kikanda katika ujenzi wa amani na kuimarisha uratibu wa EAC katika utayari na kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwamo Covid-19.

EAC imeiomba EU kusaidia mipango ya kujenga uwezo ambayo itazingatia uimarishaji wa taasisi na mabadiliko ya taasisi usimamizi wa miradi na Ufuatiliaji na Tathmini (M&E), uimarishaji manunuzi, ukaguzi na usimamizi wa mipango, bajeti na uhasibu na taratibu za usimamizi wa fedha pamoja na mfumo jumuishi wa usimamizi wa habari.

Mkuu wa Ujumbe wa EU nchini Tanzania, Balozi Manfredo Fanti alimhakikishia Dk Mathuki kuwa EU itaendelea kufanya kazi nao kwa karibu na kuipongeza Sekretarieti kwa kazi nzuri iliyowezesha kupatikana kwa mafanikio mengi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz