Mataifa sita kati ya 54 ya Afrika ni miongoni mwa nchi ambazo hazijapata maambukizi ya virusi vya corona. Ugonjwa huo wa dunia umeshathibitishwa kuwepo karibu katika kila nchi, lakini katika nchi za visiwa vilivyo mbali, Yemen ambako kuna vita na Korea Kaskazini iliyojitenga, hakuna maambukizi hayo. Mamlaka barani Afrika zinadai kuwa ni Mungu ndiye ameziepusha, au kutokana na kutokuwa na safari za ndege nyingi zinazoingia nchi hizo, lakini kuna hofu kwamba ukosefu wa vifaa vya kupimia ugonjwa huo kunaweza kuwa kunaficha uhalisia. Sudan Kusini- Taifa hilo la Afrika mashariki ambalo ndio kwanza linatoka katika kipindi cha vita iliyochukua miaka sita, likiwa na kiwango kikubwa cha njaa, magonjwa na miundombinu michache, wataalamu wanasema kunaweza kutokea mlipuko wa virusi hivyo. Daktari Angok Gordon Kuol, mmoja wa watu waliopewa jukumu la kusimamia vita dhidi ya virusi vya corona, alisema nchi hiyo ilifanya vipimo kwa watu 12 na hakuna aliyegundulika kuwa na maambukizi. Alisema sababu ya virusi hivyo kutofika Sudan Kusini inaweza kuwa ni kutokuwa na safari nyingi za ndege zinazoingia na safari nyingine za kuingia taifa hilo. "Ndege chache zinakuja Sudan Kusini na nchi nyingi zilizopata maambukizi, zilipata kutoka kwa watu wanaoingia kutoka nje." Alisema tatizo kubwa ni wageni wanaofanya kazi katika taasisi kubwa zisizo za kiserikali na jumuiya ya watoaji huduma za kibinadamu, au watu wanaovuka mipaka kutoka nchi jirani kwa kutumia usafiri wa ardhini. Sudan Kusini imefunga shule, kupiga marufuku mikusanyiko kama ya harusi, mazishi na michezo na kuzuia ndege zinazotoka nchi zenye maambukizi. Biashara zisizo na umuhimu zimefungwa. Kwa sasa nchi inaweza kupima watu 500 na ina kituo kimoja cha kuwaweeka watu wenye maambukizi au wanaohisiwa kuwa nayo.
- Burundi - Nchini Burundi, ambako wanajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Mei, mamlaka zinamshukuru Mungu kwa kutokuwa na watu wenye maambukizi ya virusi hivyo. "Serikali inashukuru nguvu za Mungu kwa kuikinga Burundi," msemaji wa serikali, Prosper Ntahorwamiye alisema katika televisheni ya taifa. Wakati huohuo, alikosoa "wanaoeneza uvumi" kuwa Burundi haina uwezo wa kupima virusi vya corona au kwamba maambukizi yanaenea bila ya kujua. Baadhi ya hatua zimechukuliwa, kama kuzuia ndege kutoka nje na kuweka sehemu za kuoshea mikono katika benki na migahawa jijini Bujumbura. Hata hivyo, madaktari kadhaa wameeleza wasiwasi wao. "Hakuna maambukizi Burundi kwa sababu hakuna upimaji," alisema daktari mmoja akitaka jina lake lisitajwe.
- Sao Tome and Principe - Sao Tome and Principe, kisiwa kidogo kilicho na misitu, hakijaripoti kuwepo kwa maambukizi kwa sababu hakina uwezo wa kupima, kwa mujibu wa mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Anne Ancia. Hata hivyo "tunaendelea na maandalizi," huku watu karibu 100 wakiwa chini ya karantini baada ya kurejea kutoka nchi ambazo zina maambukizi, na WHO inatupia jicho kwa wanaoumwa nimonia. Ikiwa na vitanda vinne tu katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) kwa watu 200,000, nchi hiyo ina hofu kubwa ya maambukizi hayo na imeshafunga mipaka yake licha ya umuhimu wa utalii katika uchumi wake.
- Malawi - Waziri wa Afya wa Malawi, Joshua Malango alipuuzia hofu kuwa Malawi inaweeza isipate wagonjwa wa Covid-19 kutokana na kutokuwa na vifaa vya kupimia: "Tuna vifaa vya kupimia nchini Malawi na tunapima." Dk Bridget Malewezi kutoka chama cha madaktari aliiambia AFP kwamba wakati "tunaweza tusiwe tayari kwa asilimia 100", serikali inajiandaa kukabiliana na virusi vya corona. Alisema kuwa ni suala la muda tu kabla ya ugonjwa huo haujaingia Malawi. "Ni kwamba katika wiki chache za kwanza maambukizi yamekuwa yakisambaa kwa kasi barani Afrika kw ahiyo watu wwengi wanaona kuwa kuna wakati maambukizi yatafika...," alisema. Malawi imetaka watu wanaoingia kutoka katika nchi zilizoathiriwa vibaya na virusi hivyo kujitenga, kitu ambacho Malawezi alisema kimesaidia kuikinga nchi dhidi ya kuenea kwa virusi hivyo.
- Lesotho - Nchi ndogo ya Lesotho, ambayo imezungukwa na Afrika Kusini na ikiwa na watu milioni 2 tu, ilizuia watu kutoka nyumbani kuanzia jana Jumatatu licha ya kutokuwa na maambukizi. Hadi wiki iliyopita, nchi hiyo haikuwa na vifaa vya kupimia au vituo vya kupimia, na ilipokea vifaa vyake vya kwanza vilivyotolewa msaada na bilionea wa China, Jack Ma. Mamlaka zilitangaza watu wanane waliokuwa wanachunguzwa kama wana maambukizi na matokeo ya kwanza yanategemewa wakati wowote.
- Comoros - Kisiwa hicho kilicho Bahari ya Hindi na kilicho kati ya Madagascar na Msumbiji, hakijatangaza kuwa na maambukizi, kwa mujibu wa wizara ya afya. Daktari mmoja jijini Moroni, Dr Abdou Ada, anashangaa kama hiyo haiwezi kuwa inatokana na matumizi ya dawa aina ya Artemisinin za kutibu malaria. "Naamini kuwa kutibu kwa kiwango kikubwa malarial kunaeleza jinsi Covid-19 ilivyoshindwa kuwapata Wacomoro, angalau kwa sasa. Ni imani yangu binafsi, hilo inabidi lithibitishwe kisayansi."