Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF, limesema idadi ya watu wasio na uhakika wa kupata maji safi na salama imeongezeka kwa kasi katika Pembe ya Afrika, huku eneo hilo likikumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 40.
UNICEF imesema leo kuwa nchini Ethiopia, Kenya na Somalia idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa maji imeongezeka kutoka milioni 9.5 hadi milioni 16.2 ndani ya miezi mitano.
Katika nchi za Afrika Magharibi na Kati za Burkina Faso, Chad, Mali, Niger na Nigeria, watoto milioni 40 wako katika hatari kubwa ya kukosa maji.
Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi ya watoto milioni 2.8 wanakabiliwa na utapiamlo mbaya katika maeneo yote hayo.
Watoto hao wana uwezekano wa mara 11 zaidi wa kufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na maji kuliko watoto wanaopata lishe bora.