Aliyekuwa Gavana wa Kiambu na rafiki wa Rais Uhuru Kenyatta William Kabogo ameonya kuwa hivi karibuni nchi itafungwa kufuatia kuongezeka kwa visa ya Covid-19.
Katika ujumbe wake Twitter, Kabogo aliwarai Wakenya kukaa macho ikizingatiwa kuwa kwa muda wa wiki chache zilizopita watu wengi wamepoteza maisha yao kutokana na maradhi hayo hatari.
"Ni bayana kwamba taifa litafungwa tena hivi karibuni, wimbi la 3 la covid-19 ni hatari," alisema.
Kumekuwa na fununu kwamba heunda Rais Uhuru Kenyatta akalihutubia taifa wishoni mwa juma kutangaza hatua mpya za kukabiliana na maambukizi ya janga la corona.
Hisia za Kabogo zinaoana na takwimu za hivi karibuni kutoka kwa Wizara ya Afya ambazo zinaonyesha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaopoteza maisha yao kutokana na makali ya virusi hivyo.
Katika siku nne tu, kutoka Jumatatu, Machi 22, hadi Alhamisi, Machi 25, vifo 81 vimerekodiwa na Wizara ya Afya.
Katibu katika Wizara ya Mercy Mwangangi alionya kuwa wengi wameonekana kupuuza masharti ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
"Iwapo tutaendelea hivi, itatulazimu kuchukua hatua kali hata zaidi ili kulinda maisha ya watu wetu," Mwangangi alisema.
Awali, TUKO.co.ke iliripoti kwamba mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alimtaka Uhuru kuweka sheria ya kutoingia au kutoka katika maeneo ambapo Covid-19 inapepea.
Akiongea na runinga ya Citizen Alhamisi Machi 25, Otiende alisema Rais anafaa kurudisha hatua kali zilizokuwa zimetolewa na serikali kukabili Covid-19.
"Ukiangalia baadhi ya maeneo kama vile Kiambu na Machakos maambukizi yako juu zaidi na ni lazima kafyu ya kutoingia au kutoka maeneo hayo ili tuyaokoe maisha ya watu wetu," alisema Otiende.
Kilio cha mbunge huyo kinajiri baada ya Wizara ya Afya kutangaza kuwa kaunti zinazokaribia Nairobi zinarekodi maambukizi mengi.
Wakati ugonjwa huo ulizuka mara ya kwanza Machi 2020, serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwamo kufunga baadhi ya kaunti.
Nairobi, Mombasa na Mandera zilikuwa baadhi ya kaunti ambazo zilifungwa wakati huo na serikali ikaweka doria barabara wakazi wasiingie au kutoka maeneo hayo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.