Miili ya watu wasiopungua 87 wanaodaiwa kuuawa na Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan imepatikana katika kaburi la halaiki, kulingana na UN.
Shirika hilo lilisema watu wa Masalit ni miongoni mwa waliozikwa kwenye kaburi lisilo na kina kirefu nje kidogo ya El-Geneina.
Mapigano makali kati ya RSF na wanajeshi wa Sudan yamekuwa yakiendelea tangu mwezi Aprili.
Lakini RSF na wanamgambo washirika wao wamekanusha kuhusika katika mapigano ya hivi majuzi huko Darfur Magharibi.
Maelfu wamefariki dunia na mamilioni wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano kati ya jeshi la kawaida la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na RSF inayoongozwa na naibu wa zamani wa al-Burhan, Mohamed Hamdan Daglo.
Umoja wa Mataifa umesema takriban miili 37 ilizikwa katika eneo la Darfur Magharibi tarehe 20 Juni, na mingine 50 katika eneo hilo hilo siku iliyofuata.
Miongoni mwa waliozikwa ni wanawake na watoto.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk alisema "amechukizwa na jinsi wafu, pamoja na familia zao na jamii, walivyotendewa" bila huruma tena kwa dharau.
Alitoa wito wa uchunguzi wa vifo vyao na kusema kwamba RSF inalazimika kuwachukulia waliokufa kwa "utu".
Mapema wiki hii, RSF ilikataa madai kutoka kwa Human Rights Watch kwamba waliwaua watu 28 wa jamii ya Masalit na kujeruhi makumi ya raia kabla ya kuharibu mji wa Misteri mwezi Mei.