Helikopta ya Umoja wa Mataifa ilitua ghafla katika eneo linalodhibitiwa wanamgambo wenye silaha nchini Somalia baada ya kugongwa na kitu, chanzo cha Umoja wa Mataifa kimesema.
Wapiganaji wa Al-Shabab walikamata helikopta hiyo, huku ripoti ambazo hazijathibitishwa zikidokeza kwamba abiria mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi, chanzo kiliiambia BBC.
Watu wengine sita waliokuwa ndani ya ndege hiyo wanazuiliwa na wanamgambo hao, huku wawili wakiripotiwa kutoroka, chanzo kiliongeza.
Helikopta hiyo ilikuwa katika shughuli ya matibabu ilipotua karibu na kijiji.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ulithibitisha "tukio la anga" siku ya Jumatano lililohusisha helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa imepewa kandarasi za huduma zake ktika sehemu hiyo.
Haikutaja al-Shabab, lakini ilisema "juhudi za kukabiliana na tukio hilo zinaendelea".
Chanzo hicho cha Umoja wa Mataifa kiliiambia BBC kuwa mmoja wa watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo ni Msomali, huku wengine wanane wakitoka kwingineko barani Afrika na Ulaya.
Raia hao wa kigeni ni pamoja na mtu aliyeripotiwa kuuawa na wawili waliofanikiwa kutoroka.Hatima yao haijulikani.
Wote tisa, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wanne, walikuwa wakandarasi na si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.Baadhi yao walikuwa madaktari, chanzo cha UN kilisema.
Helikopta hiyo ilikuwa ikielekea katika mji wa Wisil karibu na mstari wa mbele wa mashambulizi ya serikali dhidi ya al-Shabab ilipoanguka baada ya kupigwa na kitu kisichojulikana, chanzo kiliongeza.
Afisa wa jeshi la Somalia Meja Hassan Ali aliliambia shirika la habari la Reuters Jumatano kwamba ndege hiyo "ilikuwa ikibeba vifaa vya matibabu na ilipaswa kuwasafirisha wanajeshi waliojeruhiwa kutoka eneo la Galgudud".
Al-Shabab inadhibiti maeneo makubwa ya kusini na katikati mwa Somalia.
Kundi hilo lina mfungamano na al-Qaeda na limeendesha uasi wa kikatili kwa karibu miaka 20.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilichapisha kwenye mitandao ya kijamii Jumatano usiku kwamba ndege hiyo "siyo ya WFP au ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma ya Kibinadamu ya Anga na hakuna wafanyakazi wa WFP waliokuwa ndani".
WFP iliongeza kuwa kama tahadhari, safari zake za ndege katika eneo hilo zimesitishwa kwa muda.
Serikali ya Somalia katika miezi ya hivi karibuni imezidisha mapambano yake dhidi ya kundi lenye uhusiano na al-Qaeda.