Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzoa taka hatarini kunyongwa kwa kutumia simu ya kuokota

IMG 20231209 WA0003 Mzoa taka hatarini kunyongwa kwa kutumia simu ya kuokota

Sat, 9 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mzoaji taka aliyeweka simu aliyookota kwenye jaa la taka amejiunga na orodha ya wengine ambao huenda wakahukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na simu ya mwanamke aliyeuawa nyumbani kwake jijini Nairobi.

Matheka Musembi, 23, anakabiliwa na hukumu ya kifo kwa hatia ya wizi wa kimabavu baada ya kupatikana na simu ya Bi Loice Nyokabi Kingori aliyeuawa na watu wasiojulikana ndani ya nyumba yake katika Eneo la Umoja.

Mshukiwa ameshtakiwa kwa kumwibia Bi Kingori simu hiyo yenye thamani isiyojulikana kati ya Septemba 20- 23, 2023 kinyume na Kifungu 296 (2) cha Sheria.

Anashutumiwa kutekeleza uhalifu huo kwa ushirikiano na washukiwa wengine ambao hawajafikishwa kortini na kumuua Bi Kingori, hatia ambayo hukumu yake ni kifo iwapo mshukiwa atapatikana na hatia.

Musembi anakabiliwa na mashtaka ya ziada ya kupatikana na bidhaa za wizi kinyume na kifungu 32 (1) (2) cha sheria baada ya kudaiwa kupatikana na simu hiyo.

Alijiunga na washukiwa wengine wawili – Elizabeth Muthoki Kinyae, 19, na Esther Nekesa Muyaka, 18, waliokuwa wameshtakiwa awali kwa kumwibia Bi Kingori simu zake mbili na kumuua kwa kumjeruhi wakati wa kisa hicho cha wizi.

Sawa na wawili hao, Musembi alinaswa na DCI baada ya kuweka kadi yake ya mawasiliano katika simu mojawapo ya marehemu na kuanza kuitumia.

Alieleza makachero kwamba alipata simu hiyo alipokuwa akipakua taka kutoka lori lililokuwa limesafirisha taka kwenye jaa la Dandora, Nairobi, karibu miezi miwili iliyopita.

Mshukiwa alitupa laini aliyopata ndani ya simu hiyo baada ya kushauriana na familia na marafiki zake kabla ya kuanza kuitumia ambapo alikamatwa.

Washukiwa hao watatu sasa huenda wakaadhibiwa kwa mauaji ambayo hawajui chochote kuyahusu baada ya kubainika kuwa simu walizopatikana nazo ziliibwa kutoka kwa mhasiriwa.

Bi Kingori alipatikana akiwa ameaga dunia langoni pake mnamo Septemba 23, na dada yake aliyekwenda kumjulia hali alipokosa kujibu simu zake, jambo ambalo halikuwa la kawaida kabla ya simu zake mbili kuzimwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live