Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzee wa miaka 70 ashitakiwa kwa kukataa kuchukua kitambulisho cha taifa

Muchina Mzee wa miaka 70 ashitakiwa kwa kukataa kuchukua kitambulisho cha taifa

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mzee mwenye umri wa miaka 70 ameshtakiwa kwa kukataa kuchukua kitambulisho cha kitaifa na wizi wa Ksh 362,000 (sawa na Tsh milioni 5.9).

Stanley Nguriathi Muchina alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani Gilbert Shikwe kwa “kukataa kuchukua kitambulisho ilhali amepitisha umri wa miaka 18.”

Alishtakiwa kwamba mnamo Agosti 14, 2023, katika kijiji cha Kinoo, Kaunti ya Kiambu alipatikana na polisi akiwa hana kitambulisho ilhali alikuwa amehitimu umri wa kuchukua kitambulisho.

“Ulipatikana na polisi ukiwa huna kitambulisho ilhali wewe umehitimu umri wa kujiandikisha na kuchukua kitambulisho,” mshtakiwa alifahamishwa na Bw Shikwe.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo sawia na shtaka la pilli kwamba aliiba zaidi ya Tsh milioni 5.9.

Mahakama ilifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Judy Koech kwamba pesa hizo zilikuwa mali ya kampuni ya East Coast Horizon Limited.

Shtaka lilisema mshtakiwa aliiba pesa mnamo Agosti 26, 2023, katika afisi za shirika la Postal Corporation katika jengo la General Post Office (GPO). Jengo hilo la GPO liko kwenye barabara ya Koinange, Nairobi.

Bw Muchina alikanusha mashtaka dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana akisema “ni mtumishi wa umma aliyestaafu.”

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Mimi ni Mzee niliyestaafu kutoka utumishi wa umma na sina mapato hata!” Bw Muchina alimsihi hakimu.

Bi Koech hakupinga ombi hilo la dhamana ila aliomba korti izingatie pesa hizo ziliibwa kutoka GPO.

Akitoa uamuzi, hakimu alimwamuru mshtakiwa awasilishe dhamana ya Ksh400,000 (Tsh milioni 6.5) na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Pia hakimu alimweleza mshtakiwa anaweza kulipa dhamana ya badala ya Tsh milioni 3.3 pesa taslimu akishindwa kupata dhamana ya Tsh milioni 6.5. Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 27, 2023, kutengewa siku ya kusikilizwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live