Mwili wa mfanyabiashara kutoka Kaunti ya Nandi aliyeaga dunia katika hali tatanisha miaka mitatu iliyopita, umelazimika kufukuliwa kinyume na kanuni za dini ya Kiislamu kufuatia mvutano kuhusu urithi wa mali yake.
Mwili wa Fahiye Muhammud Ahmedin ulifukuliwa Ijumaa asubuhi kutoka makaburi ya Kiislamu ya Kapsabet na maafisa wa Iwale wa kitaalamu wa serikali chini ya ulinzi mkali, katika mchakato wa kuchunguza mauaji yake.
Ufukuzi huo ulitokana na mvutano kuhusu mrithi halali wa marehemu; baina ya mamake na mjane wake. Suala kuhusu baba mzazi ndicho kiini cha mvutano huo huku mama akidai marehemu alikuwa amewakana watoto wake.
Fahiye alipatikana ameaga dunia nyumbani kwake Septemba 12, 2020 huku taarifa ya polisi ikiashiria kwamba alijitia kitanzi.
Licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya familia, maiti hiyo ilizikwa upesi siku mbili baada ya kifo chake kuambatana na desturi za Kiislamu.
Mamake marehemu, Bi Zeinab Hammed, alikuwa nchini Zambia mwanawe alipofariki na aliporejea nyumbani alianza mchakato wa “kusaka haki kuhusu mtoto wake.”
“Tulikuwa tunawasiliana na Fahiye kila wakati kabla ya kifo chake. Alilalamikia tofauti kali baina yake na mkewe, ikiwemo mvutano kuhusu baba halisi aliyezaa watoto wao. Aliwahi nifichulia siri kwamba watoto hao watatu si wake na alishuku walizaliwa nje ya ndoa,” akadai Bi Hammed.