Kiongozi wa kitamaduni nchini Zimbabwe ameaamuru kwamba mabaki ya rais wa zamani wa nchi hiyo Robert Mugabe yafukuliwe na kuzikwa katika makaburi ya kitaifa.
Mugabe alifariki mwaka 2019 na alizikwa nyumbani kwake Kutama kulingana na ombi lake na wala sio katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa katika mji mkuu, Harare, kama alivyotarajia mrithi wake Rais Emmerson Mnangagwa na wengine.
Familia yake imesema Mugabe alikuwa ameelezea hofu yake kwamba mahasimu wake wa kisiasa waliomuondoa madarakani mwaka 2017 huenda wakatumia mabaki yake kufanya kafara ikiwa atazikwa katika makaburi ya kitaifa.
Siku ya Jumatatu, chifu wa kitamaduni katika wilaya ya Zvimba, magharibi mwa mji mkuu wa Harare, alisema kwamba amepokea malalamishi kutoka kwa jamaa wa ukoo wa Mugabe kuhusu mahali alipozikwa.
Aliamua kuwa Grace Mugabe alikuwa na makosa kwa kukiuka muongozo wa kimila kwa kumzika mume wake nyumbani kwake. Mugabe hakufika mbele ya kikao hicho, lakini chifu alimpiga faini ya kulipa ng’ombe watano na mbuzi mmoja.
“Yeye [chifu] hana mamlaka dhidi ya Kutama. Na hata kama chifu alifanya uamuzi sahihi tungelikata rufaa mahakamani,” Leo Mugabe, msemaji wa familia, aliliambia Shirika la Habari la Reuters.