Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili aliyejinyonga gerezani Kenya kurejeshwa Tanzania

036921105f93cb77b84a7c9bba9fd1d4 Mwili aliyejinyonga gerezani Kenya kurejeshwa Tanzania

Tue, 8 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI ya Kenya imekubali kutoa kibali kwa familia ya marehemu Rashid Mberesero cha ruhusa ya kupewa mwili wa kijana wao aliyejinyonga wiki iliyopita katika Gereza la Kamiti nchini Kenya wakati akitumikia kifungo cha maisha.

Rashid Mberesero alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kukutwa na hatia ya kushiriki katika shambulizi la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya, Aprili 2015 na kuua wanafunzi zaidi ya 150.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Talha Mohammed aliliambia HabariLEO jana kuwa, baada ya kupokea maombi ya familia ya kutaka mwili wa kijana wao, Serikali ya Kenya ilitoa kibali mara moja na tayari ubalozi umeitaarifu familia ya Mberesero.

Alisema familia hiyo inatarajiwa kufika Nairobi nchini Kenya leo au kesho. Kwa mujibu wa Talha, wanafamilia watakapofika, watakabidhiwa mwili wa kijana wao tayari kwa kuusafirisha hadi Same mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

Alisema ubalozi uliyapeleka maombi hayo kwa wakati na Serikali ya Kenya ikakubali kuuachia mwili huo kwa familia kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika eneo la Gonja wilayani Same katika Mkoa wa Kilimanjaro.

“Mpaka sasa familia ilishajulishwa kuhusu ruhusa hiyo na tunavyozungumza wako njiani kuja Kenya; nafikiri wanaweza kuingia kesho (leo) au keshokutwa (kesho) hapa Nairobi kwa ajili ya kuchukua mwili huo kwa ajili ya mazishi Tanzania,” alisema.

Baba mzazi wa Rashid, Charles Mberesero, alisema familia inaendelea na maandalizi ya kuchukua mwili kutoka Kenya baada ya taratibu zote kukamilika.

Alisema baada ya kupewa mwili huo wa kijana wake, wanatarajia kuzika eneo la Gonja kwa kuwa alikulia huko kwa mama yake wakati nyumbani kwa baba ni Mwanga mkoani humo.

Kwa mujibu wa baba huyo, kijana huyo akiwa gerezani alikata rufaa bila familia kujua na wakati tarehe ya kusikilizwa kwa rufaa yake ikikaribia, inasemekana alijiua kwa kujinyonga akiwa gerezani.

Rashid, kijana aliyekuwa akisoma katika Shule ya Sekondari ya Kigwe mkoani Dodoma, alisafiri kwenda Kenya akitokea shuleni bila familia kujua kabla ya kupata taarifa kuwa amekamatwa nchini Kenya kwa tuhuma za kujihusisha na ugaidi.

Alihukumiwa pamoja na wenzake wawili, Hassan Edin na Mohamed Abdi raia wa Kenya waliofungwa kifungo cha miaka 41 kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika shambulio la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa Aprili 2015.

Wakati wa shambulio hilo, magaidi waliwauwa kwa kuwapiga risasi wanafunzi zaidi ya 500 ambapo 150, kati yao ndio waliothibitika kufa.

Vijana hao watatu walitiwa hatiani kwa kula njama na kufanya shambulio la kigaidi kwa kushirikiana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye maskani yake Somalia.

Kundi hilo limehusika katika matukio kadhaa nchini Kenya likiwemo la West Gate ambapo magaidi waliwauwa wananchi wa Kenya zaidi ya 60 na kujeruhi wengine mamia.

Chanzo: habarileo.co.tz