Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwandishi wa habari wa Runinga Somalia auawa katika shambulio la kujitoa mhanga

Mwandishi Wa Habari Wa Runinga Somalia Auawa Katika Shambulio La Kujitoa Mhanga Mwandishi wa habari wa Runinga Somalia auawa katika shambulio la kujitoa mhanga

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: Bbc

Risala za rambirambi zimetolewa kwa mwandishi wa habari maarufu wa TV ya Somalia baada ya kuuawa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika mgahawa mmoja katika mji mkuu, Mogadishu.

Abdifatah Moalim Nur, maarufu kama Qeys, alielezewa na wenzake kama mtu "wa kipekee" na "mwenye ushawishi.

Anakuwa mwanahabari wa kwanza kuuawa nchini Somalia mwaka huu, kulingana na shirika la uangalizi wa vyombo vya habari nchini humo.

Kundi la wanamgambo wenye uhusiano na al-Qaeda, al-Shabab, lilisema lilifanya shambulio la kujitoa mhanga katika mgahawa wa Blue Sky.

Polisi walisema watu wengine wanne walijeruhiwa nje ya mgahawa huo ambao uko karibu na ikulu ya rais.

Muungano wa Kitaifa wa Waandishi wa Habari wa Somalia (NUSOJ) ulisema "umetikiswa sana" na mauaji ya "kipumbavu na ya kikatili" ya Nur, mkurugenzi wa Televisheni ya kibinafsi ya Somali Cable.

"Kazi yake ya ajabu na kujitolea kwake kumeacha alama isiyofutika katika uandishi wa habari wa Somalia, na kuwatia moyo waandishi wengi wachanga kujitahidi kwa ubora," umoja huo ulisema.

Nur, mtetezi mkuu wa uhuru wa vyombo vya habari, hapo awali alikabiliwa na vitisho, Shirika la Wanahabari wa Somalia (SJS), lilisema.

Mwezi Oktoba mwaka jana, mwanahabari Mohamed Isse Hassan alikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 100 waliouawa katika milipuko miwili ya magari mjini Mogadishu.

Mwezi mmoja kabla, ripota wa Televisheni ya Taifa ya Somalia inayomilikiwa na serikali, Ahmed Mohamed Shukur, aliuawa na bomu lililotegwa ardhini karibu na mji mkuu.

Chanzo: Bbc