Mtangazaji maarufu wa redio na mmoja wa waandishi wanaotajwa kuwa na msimamo wa kuikosoa serikali ya Cameroon, Martinez Zogo amekutwa amekufa kufuatia kutoweka kwake Jumanne ya wiki iliyopita kwa kinachodhaniwa kuwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Zogo alikuwa mkurugenzi wa kituo binafsi cha redio cha Amplitude FM na alikuwa akiendesha kipindi maarufu cha “Embouteillage”.
Siku za karibuni alikaririwa kwenye kipindi chake akizungumzia ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma uliowahusisha baadhi ya wafanyabiashara matajiri sambamba na viongozi wa juu wa serikali ya nchi yake.
Msemaji kutoka kituo hicho cha redio amesema kuwa mbali ya mwili wa mke wa Zogo pia wamegundua mwili wa mtangazaji wa redio ambao ulikuwa umtelekezwa kwenye viunga vya mji mkuu wa Cameroon, Yaoundé.
Kikundi cha wanaharakati wa haki za waandishi wa habari kimesema kuwa jeshi la polisi nchini Cameroon lilisikia makelele makubwa nje ya kituo chao usiku wa Jumanne iliyopita na wakagundua gari iliyoharibiwa vibaya ya Martinez Zogo.
Gari ndogo nyeusi ilionekana ikiondoka kwenye eneo hilo.