Mwili wa mwanamume aliyekuwa ametoweka kwa siku tano ulipatikana ukiwa umeanza kuoza katika nyumba yake huko Kayole, Nairobi.
Polisi walisema mtu huyo, 40, alikuwa hajaonekana tangu Februari 25. Mwili wake ulipatikana katika nyumba yake ukining'inia kwenye paa na kamba shingoni.
Majirani walikuwa wamelalamika kuwa kulikuwa na harufu mbaya kutoka kwa nyumba hiyo na walipochungulia kupitia dirishani, waliona mwili huo. Polisi waliitwa wakauchukua na kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi wa maiti.
Mkuu wa polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema uchunguzi wa awali waonyesha kuwa mwanamume huyo alifariki kwa kujitoa uhai siku ambayo alionekana mara ya mwisho kwani mwili wake ulikuwa umeharibika kwa kiasi kikubwa.
"Nia ya kujiua bado haijajulikana hadi sasa," alisema.
Huko California, Eastleigh, mwili wa mwanamke ambaye hakutambulika ulipatikana karibu na uzio wa kambi ya kijeshi. Wafugaji waliokuwa wakichunga mifugo yao katika eneo hilo waliripoti kuona mwili huo na kupiga simu polisi.
Polisi walisema mwanamke huyo alionekana kuwa na umri wa takriban miaka 25 na aliuawa kwingine na mwili huo kutupwa katika eneo la tukio. Mwili huo ulikuwa na kipande cha nguo shingoni mwake na inashukiwa alinyongwa.
Polisi walisema pia kulikuwa na dalili za kukabwa koo huku kukiwa na jeraha kwenye paja la mguu wa kushoto. Mwili huo ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri kutambuliwa na uchunguzi wa maiti kufanywa ili kubaini kilichosababisha kifo chake.
Polisi walisema hakuna mtu aliyekamatwa lakini wanachunguza tukio hilo.