Watu wenye silaha nchini Eswatini wamemuua mwanasiasa mashuhuri wa upinzani na mwanasheria wa haki za binadamu nyumbani kwake, msemaji wa chama chake ameiambia AFP jana Jumapili, saa chache baada ya mfalme wa nchi hiyo kuwashutumu wanaharakati wanaopinga utawala wake.
Thulani Maseko aliuawa kwa kupigwa risasi Jumamosi usiku na washambuliaji wasiojulikana huko Luhleko, umbali wa kilomita 50 na mji mkuu Mbabane, msemaji wa chama cha upinzani Sikelela Dlamini amesema.
Msemaji huyo amesema aliambiwa “ wauaji walimpiga risasi kupitia dirisha akiwa ndani ya nyumba na familia yake”.
Serikali ilituma salamu za rambirambi kwa familia yake, ikisema kifo cha Maseko ni “hasara kwa taifa” na kwamba polisi wamekuwa wakiwasaka waliomua.
Maseko alikuwa mwanasheria kiongozi wa haki za binadamu na mwandishi wa maoni nchini Eswatini, ambaye alikuwa na kesi inayoendelea mahakamani dhidi ya uamuzi wa Mfalme Mswati wa tatu kubadili jina la nchi na kuipa jina la Eswatini kwa amri.
Jina la nchi lilibadilishwa kutoka Swaziland na kuitwa Eswatini kwa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka wa 2018.
Msimamo wa Maseko ulikuwa kwamba Mfalme hakufuata utaratibu wa katiba.