Makachero wa upelelezi wa jinai DCI wamemtia mbaroni mwanamume mmoja anayetuhumiwa kumbaka ajuza wa miaka 77 ambaye ni mwendawazimu.
Joseph Muema, mwenye umri wa miaka 45, kwa sasa yuko kizuizini kufuatia kukamatwa kwake kwa kitendo cha kuchukiza kilichowashangaza wakazi wa kijiji cha Ikuuni eneo la Kindaruma, DCI waliripoti.
Hapo awali, mshukiwa alidaiwa kuingia kinyemela katika chumba cha kulala cha mwathiriwa mwenye umri wa miaka 77 kabla ya kunaswa na mtoto wa mwathiriwa, ambaye alikuwa ameenda kumtazama mamake mwendo wa saa tano usiku.
Baada ya kufumaniwa na kijana wa ajuza huyo, Muema aliruka na kuchana mbuga kusikojulikana na baada ya ripoti kupigwa, msako dhidi yake ulianzishwa mara moja kuanzia usiku wa Jumanne.
“Kufika kwa mtoto huyo kulimfanya Muema kutoroka na kusababisha kukimbizwa, lakini mwanawe ajuza huyo alizidiwa nguvu na mshukiwa aliyekimbia na kumfanya aite polisi kwa usaidizi. Kwa bahati nzuri, mshukiwa alikuwa ameacha suruali yake na kanda mbili za miguuni, na hivyo kurahisisha upekuzi kumtafuta asubuhi na mapema,” sehemu ya ripoti ya DCI ilisoma.
Mshukiwa na mwathiriwa walisindikizwa hadi hospitali ya Mbiuni level 4 ambapo vipimo vya afya vilithibitisha kuwa mwathiriwa alibakwa.