Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 33, raia wa Kenya ambaye alifariki dunia wiki mbili tu baada ya kuwasili Dammam nchini Saudi Arabia, anaaminika kufariki dunia kutokana na mwajiri wake kumtoa figo yake moja.
Rose Atieno aliwasili nchini Saudi Arabia mnamo Mei 23, 2022, na aliripotiwa kufariki dunia Juni 7, 2022.
Kulingana na mumewe marehemu, Abdulrazik Juma, alidai kuwa mke wake Rose Atieno alipiga simu kumfahamisha kuwa mwajiri wake alimlazimisha kufanyiwa upasuaji wa kutoa moja ya figo yake ambayo ingetolewa kwa mmoja wa jamaa yao aliyekuwa akiugua.
"Sikuweza kumpata kwa zaidi ya siku tatu. Simu yake ilikuwa imezimwa na siku tano baadaye, alinipigia kwa namba tofauti na kuniambia kuwa ametekwa nyara na amelazwa katika hospitali ili kutoa figo yake kinyume na matakwa yake," alisema.
K24 inaripoti kuwa Juma hakuweza kuwasiliana tena na mke wake na baadaye, ni rafiki yake ndiye alimfahamisha kuwa aliaga dunia katika hospitali ambako alikimbizwa baada ya kudaiwa kuanguka kutoka kwenye ngazi akisafisha madirisha nyumbani kwa mwajiri wake.
Mume wa marehemu aliongeza kuwa mwili wa Ateno uliwasili nchini Kenya Jumanne, Julai 26, usiku katika Uwanja wa Ndege wa Moi na ulipokelewa na familia.
“Mwili ulipowasili nchini na kupelekwa nyumbani kwa mkesha wa usiku nilipata muda wa kumuomboleza mke wangu na kumtazama kwa karibu mwili wake na kukuta alama za upasuaji tumboni mwake zinathibitisha vya kutosha kuwa alifanyiwa upasuaji kabla ya kufariki katika mazingira yasiyoeleweka," aliongeza.