Kisa kisicho cha kawaida kilishuhudiwa katika eneo la Kuria Magharibi Kaunti ya Migori wakati jamaa mmoja mshukiwa wa wizi wa pikipiki alikuwa anakimbizwa na wenzake kwa tuhuma za kuiba pikipiki.
Mshukiwa huyo Mwita Marwa mwenye umri wa miaka 45 aliona umauti ukimkodolea macho na kwa haraka dhamiri zake zikamtuma kukimbia katika hospitali moja na kujitosa moja kwa moja ndani ya chumba cha kujifungua kina mama.
Kulingana na DCI, hatua hii ya kuingia kwenye chumba cha leba iliwazuia wanabodaboda hao wengi ambao walikuwa wanamfuata kwa ghadhabu wakiwa na vifaa kali tayari kumsafirisha jongomeo.
“Wakiwa wamechanganyikiwa kati ya kumwachilia mshukiwa kwa watu waliokasirika au kuwa naye katika kituo hicho wakati huo mgumu, wauguzi waliokuwa zamu walichagua kuokoa maisha ya mwanamume huyo kutoka kwa umati wa watu wenye kiu ya kumwaga damu ambao ulikuwa ukitishia kuingia hospitalini.
Kwa bahati nzuri, kikosi cha askari polisi waliokuwa wakishika doria katika mji huo walisikia zogo hilo na kukimbilia eneo la tukio huku kundi hilo likitishia kuichoma moto hospitali hiyo,” sehemu ya ripoti ya DCI ilisoma.
Polisi hao kwa haraka waliingia ndani ya leba na kumpaka mshukiwa yuko chini ya huruma ya wauguzi na kina mama wajawazito.
Kwa kutumia busara ya mfalme Suleiman, polisi waliamua kumwachilia aondoke zake kupitia shimo la paa la hospitali hiyo ili kuzuia zogo na vuruga nje endapo wangetoka naye kwa kundi hilo la wanabodaboda waliokuwa na hasira za mkizi.
Polisi walipokuwa wanaodoka katika hospitali hiyo, vijana wa boda boda nje walitaka gari lisimame wakidhani ‘mteja’ wao yuko ndani lakini walipigwa na butwaa kutomuona, jambo lililowafanya kulitupia gari la polisi mawe.
“Hili liliwafanya maafisa hao kutupa vitoa machozi kwa nia ya kutawanya umati na kurejesha hali ya kawaida. OCS wa Kehancha alipata majeraha kwenye kifundo cha mguu wake wa kushoto alipokuwa akiwaongoza maafisa wake katika shughuli hiyo. Ambulensi ya hospitali hiyo pia iliharibiwa kwa kiasi kikubwa na madirisha kadhaa katika jengo kuu la hospitali hiyo yalivunjwa.”