Mivutano inaongezeka nchini Botswana kati ya jamii ya watu LGBTQ na jamii ya kikristo ya waumini wa kanisa la kiinjilisti ambalo limeandaa maandamano Jumamosi wakipinga mswaada ambao unaweza kuharamisha mahusiano ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Uamuzi wa Mahakama Kuu wa mwaka 2019 uliunga mkono haki za mashoga nchini Botswana, na kusababisha upinzani kutoka katika makundi ya kihafidhina. Mivutano inayoendelea imekuja kabla ya mjadala katika Bunge la Taifa unaotarajiwa kuanza wiki hii kujadili mswaada huo wenye utata.
Lakini wanachama wa jumuiya ya mashoga hawafurahishwi na juhudi za viongozi wa kidini katika kuwashawishi wabunge.
Thato Moruti ambaye ni mtendaji mkuu wa kundi la LGBTQ nchini Botswana, au LEGABIBO amesema, "Ninaamini kuwa kanisa linaweza likawa linaanzisha mwenendo hatari sana kwa kuwahadaa wabunge na mahakama," Moruti alisema. "Ni muhimu tufahamu kwamba tunaelewa kuwa hatua ya kanisa inaweza kusababisha hali ambayo itavuruga demokrasia nchini kwa sababu wanajaribu kusukuma msingi huu wa kikristo kwa Batswana.” Moruti alisema kuwa kuna haja ya kutafuta muafaka badala ya malumbano kati ya kanisa na jumuiya ya mashoga.
Akikabidhi ombi bungeni wakati wa maandamano ya mwishoni mwa wiki, mwenyekiti wa Evangelical Fellowship ya Botswana Pulafela Siele aliwataka wabunge kupiga kura ya kuupinga mswaada huo.
"EFB inaamini kwamba ikiwa bunge litachukua hatua kama inavyotakiwa na mswada huo, hatua hiyo itafungua milango ya uasherati na kusababisha mambo ambayo hayakubaliki katika taifa kama vile ndoa za jinsia moja, mabadiliko ya mitaala ya shule ili kuwafundisha watoto wetu vitendo hivyo," alisema Siele.
Mwaka 2019, mahakama kuu ya Botswana ilipitisha sheria kwamba kuharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha katiba. Tshiamo Rantao, wakili aliyewakilisha jumuiya ya Mashoga katika kesi ya mwaka 2019, alisema bunge halina mamlaka ya kujadili mswaada huo, lakini badala yake lazima liheshimu uamuzi.
Lakini mbunge Wynter Mmolotsi, ambaye alipokea ombi hilo kwa niaba ya Bunge la Kitaifa, aliiambia VOA kwa sasa ni juu ya bunge kufanya uamuzi.