Maafisa wa serikali ya Algeria wamezuia uingizaji wa wanyama hai kutoka Ufaransa baada ya kugunduliwa ugonjwa wa virusi katika mifugo ya Ufaransa.
Mivutano ya kisiasa kati ya Algeria na Ufaransa imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, haswa katika mwaka uliopita kutokana na misimamo na hatua za Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.
Waalgeria ambao waliteseka kwa miaka mingi kutokana na ukoloni wa Ufaransa nchini kwao, katika miaka ya hivi karibuni, wamepaza sauti zaidi kupinga dhulma na siasa za ukoloni mamboleo za Paris baada ya kufichuliwa nyaraka zaidi zinazohusiana na jinai zilizofanywa na Wafaransa nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anatolia, Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Vijijini ya Algeria imetangaza katika taarifa yake kwamba, uamuzi huo wa kupiga marukufu uingizaji wa wanyama hai kutoka Ufaransa umechukuliwa baada ya kugundulika ugonjwa wa virusi unaojulikana kama homa ya kuvuja damu (hemorrhagic fever) ambao umeenea kwa ng'ombe na ndama hai nchini Ufaransa.
Mamlaka ya Ufaransa ilitangaza hadharani habari hiyo ya kugunduliwa homa ya kuvuja damu kwa wanyama nchini humo siku mbili baada ya ugonjwa huo kutambuliwa katika mikoa ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa umekuwa ukisuasua, na katika miaka ya hivi karibuni, kumefichuliwa nyaraka mpya za uhalifu uliofanywa na Ufaransa nchini Algeria, ambazo zinaanika zaidi ukatili na unyama wa Wafaransa dhidi ya wapigania uhuru wa Algeria.
Jinai za Wafaransa nchini Algeria Kwa mujibu wa mojawapo ya nyaraka hizo, zaidi ya Waalgeria milioni moja na nusu waliuawa wakati wa ukoloni wa Ufaransa na vita vya kupigania uhuru wa nchi hiyo.