Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua zinavyoacha athari Kenya, mamia wakipoteza maisha

Idadi Ya Vifo Kutokana Na Mafuriko Kenya Imeongezeka Mvua zinavyoacha athari Kenya, mamia wakipoteza maisha

Wed, 6 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko ya El Nino nchini Kenya imeongezeka hadi 160, huku watu 529,120 wakilazimika kuhama makazi yao.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ametangaza kuwa: "Msukumo wa pamoja wa kusambaza vifaa muhimu, vikiwemo vyakula na vitu visivyo vya chakula, unaendelea kwa njia ya barabara na anga huku misaada ikidondoshwa kwa ndege katika maeneo yasiyofikika katika kaunti 19 zilizoathiriwa. Juhudi za uokoaji pia zinaendelea kwa kuhusisha boti za Jeshi la Wanamaji la Kenya na Huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya.

Katika kukabiliana na maafa hayo, serikali imelazimika kuanzisha kambi tisa za ziada katika Kaunti za Tana River, Migori, Homa Bay na Voi kama njia ya kuwashughulikia watu waliokimbia makazi yao na wanaokabiliwa na athari za mafuriko.

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Kenya zimeibua changamoto nyingi, huku mafuriko yakienea, sambamba na maporomoko ya udongo kusababisha uharibifu kote nchini.

Msemaji wa serikali ya Kenya amesema athari kwa miundombinu ni kubwa, na barabara nyingi hazipitiki, zinatatiza usafirishaji wa watu na juhudi za kutoa msaada. Hali baada ya mafuriko nchini Tanzania

Huki hayo yakijiri Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiomba jumuiya za kimataifa na taasisi za ndani kusaidia juhudi za serikali ya nchi hiyo za uokoaji na kutafuta maiti wa maporomoko ya tope pamoja na misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Mwito huo uko kwenye taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania huku taarifa nyingine zikisema kuwa, idadi ya waliofariki kutokana na maafa ya mvua zilizosababisha mafuriko na maporomoko ya tope imekaribia watu 70 na zaidi ya watu 116 wamejeruhiwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Jumanne.

Taarifa zinasema mafuriko ambayo yamekumba maeneo ya Afrika Mashariki kufuatia wiki kadhaa za mvua kubwa yameua zaidi ya watu 350 na wengine milioni 1 kuwa wakimbizi katika nchi za Somalia, Kenya, Ethiopia na Tanzania.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live