Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Museveni kufikisha miaka 40 madarakari, nani kumrithi? Uchambuzi...

Museveniii Museveni kufikisha miaka 40 madarakari, nani kumrithi? Uchambuzi...

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: BBC

Uganda inaadhimisha miaka 60 ya uhuru wake, ikiwa ni moja ya nchi zilizotawaliwa na rais mmoja kwa miaka mingi zaidi, na huwenda wengi wakajiuliza je ni nani atakayeiongoza Uganda baada ya Rais Yoweri Museveni kumaliza muhula wake?

Wakati raia wa Uganda watakapofanya uchaguzi mkuu ujao mwaka 2026, Rais Museveni atakuwa ameshika hatamu za uongozi wa taifa hilo la mashariki mwa Afrika kwa miaka 40 kamili.

Katika mazungumzo baina ya Waganda ya ana kwa ana na yale ya mitandao ya kijamii mjadala juu ya mabadiliko ya uongozi wa nchi hiyo umekuwa ukijitokeza mara kwa mara, huku baadhi wakitaka Rais Museveni aondoke mamlakani, huku wanaomuunga mkono wakisema anafaa kuendelea kuhudumu.

Baadhi ya waganda hususan vijana waliozaliwa akiwa mamlakani wamekuwa wakidai kuchoshwa na utawala wake, wanaoulaumu kwa ukosefu wa ajira na umasikini. Hatahivyo wapo wafuasi sugu vijana wanaomuenzi, baadhi yao akiwaita wajukuu ama 'buzzukulu' kwa lugha ya Kiganda.

Hakuna dalili zinazoonyesha kuwa Bw Museveni ambaye atakuwa na umri wa miaka 81 mwaka 2026, anaweza kuondoka mamlakani kwa hivyo huwenda bado akajitokeza tena kugombea urais, anasema Dkt. Masereka Levi Kahaika, Mhadhiri wa na mchambuzi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Makerere.

"Mfumo wa uchaguzi wenyewe hauko sawa…sheria za uchaguzi wanaozitunga ni watu wanaoteulia na Museveni mwenyewe, sioni ikiwa Museveni anataka bado kuendelea kubaki mamlakani kuna mtu mwingine atakayeweza kuiongoza Uganda…ninaweza kusema labda uwe ni muujiza Museveni hawezi kuondoka mamlakani," anasema Maseruka, mhadhiri wa chuo Kikuu cha Makarere, ameiambia BBC.

Siku za hivi karibuni Museveni mwenyewe amekwishasema kuwa atagombea tena urais. ‘Mfumo wa viongozi wanaotumiwa na Museveni’ Ni nadra kusikia kuhusu mfumo wa utawala anaotumia rais Museveni katika kuhakikisha anabakia mamlakani.

Maafisa wanaowakilisha serikali ya Museveni katika ngazi ya wilaya wenye cheo cha Afisa Utawala Maalum wa Wilaya ( Special District Administrator), ni nguzo kuu ya utawala wa serikali ya Uganda, wakiwa jicho la rais katika ngazi za wilaya.

Kulingana na katiba ya 1995 Wakuu hawa wa wilaya waliingizwa kuwa sehemu ya utawala wa Museveni, na kulingana na katiba huteuliwa moja kwa moja na rais kwa ajili ya kufuatilia shughuli na kusimamia usalama katika wilaya.

Jukumu lao ni kwa ujumla lilikuwa ni kuwa ‘macho’ na masikio ya rais katika wilaya, lakini wamekuwa zaidi ya hilo.

"Unajua viongozi hawa hawana utendaji mbaya, lakini lazima watekeleze matakwa ya mkubwa wao rais Museveni, hilo ndio linalowafanya watekeleze zaidi ya majukumu yao, ni watu wake, wengine wanataka maslahi.

"Wakati wa uchaguzi wanafanya zaidi ya majukumu yao kuhakikisha mwajiri wao anaendelea kubakia madarakani," aliiambia makala hii Lev Maseruka Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda Maseruka.

Maafisa hawa wanadaiwa kufanya ujasusi, kukusanya taarifa na kuwa watendaji wakuu. Si ajabu kwa kwao kupokea simu moja kwa moja kutoka rais kujadili suala la usalama.

Udhibiti huu mkali wa usalama, unaelezewa na wachambuzi wengi kuwa unaonyesha jinsi Bw Museveni anavyokataa kukubali nchi itawaliwe kidemokrasia na badala yake kukumbatia utawala wake wa asili wa kijeshi.

‘Mbinu ya vitisho na kamata kamata ya upinzani’ Si ajabu Bw Museveni akatumia mbinu ya vitisho, mateso na kamata kamata dhidi ya wapinzani wake kurejea tena mamlakani.

Tangu kurejea kwa demokrasia ya vyama vingi mwaka 2005, suala la usalama limekuwa likitumiwa kuzuia juhudi za uhamasishaji wa kisiasa, jambo lililopelekea kumamatwa na kupigwa kwa wanasiasa wa wapinzani na wafuasi wao.

Kwa mfano wanasiasa wa upinzani waliogombea urais dhidi ya museveni- Kiza Besigye na Bobi pamoja na wafuasi wao, walikabiliwa na kipindi kigumu katika kampeni za uchaguzi.

Katika chaguzi zote zilizofanyika Uganda tangu mwaka 1996, Museveni amekuwa akitumia nafasi yake kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa taifa hilo kuwadhibiti wapinzani wake.

Amekuwa akitumia vyombo vya dola-polisi, jeshi na askari wengine wa vikosi visivyo rasmi kuwatisha na kuwapiga washindani wake.

Watu wanafanya kampeni, kura zinapigwa na vyama na wagombea binafsi wameruhusiwa kikatiba lakini mfumo mzima unampendelea mtawala aliye madarakani.

Karata ya 'kustaafu ya Museveni' Katika kila muhula wa utawala wake wa zaidi miongo mitatu, Bw Museveni amekuwa akionyesha dalili kwamba anajiandaa kustaafu. Mara kwa mara Museveni amekuwa akisema kwamba uchaguzi ujao utakuwa ndio uchagzui wake wa mwisho na kwamba ana ndoto ya kuishi maisha rahisi ya kuchunga ng’ombe.

Hii imemruhusu Museveni kucheza karata ya kuwapambanisha wanachama ndani ya chama chake cha NRM.

'Je ni Muhoozi Kainerugaba?' Kwa miaka mingi, kumekuwa na ripoti nyingi kuhusu mpango wa kiongozi huyo mkongwe wa kumrithisha madaraka mwanaye wa kiume Muhoozi Kainerugaba, ambaye sasa ana umri wa miaka 48, Jenerali katika jeshi atakuwa rais .

Mara kadhaa Museveni na mwanaye Muhoozi wameashiria nia ya kuendeezwa kwa urithi wa familia ya Museveni nchiniUganda.

Lakini ujumbe wa Twitter uliotangaza kustaafu kwa Muhoozi Kainerugaba kwa mwana peke wa kiume wa Rais museveni kutoka jeshi la nchi hiyo (UPDF) ambalo amelitumikia tangu mwaka 1999, uliibua hisia miongoni mwa Waganda na watu wengine kwamba huenda anajiandaa kumrithi baba yake, licha ya kwamba baadaye walitoa taarifa iliyosema Mohoozi hajiuzulu.

Ingawa Muhoozi alisema kuwa hatastaafu kabla ya miaka minane, ujumbe wake ilichochea mtizamo miongoni mwa umma wa Waganda kuwa huenda anatanga nia zake za kujitupa ndani ya siasa za Uganda.

Tetesi zaidi kuhusu uwezekano wa Mohoozi wa kumrithi baba yake kama rais wa Uganda zilivuma zaidi wakati alipoamua kuandaa sherehe ya kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa, sherehe iliyojumuisha msururu wa matukio mbali mbali ya kitaifa, ambayo kilele chake kilikuwa ni hafla ya kitaifa kalamu ya chakula cha jioni cha wanachama wafuasi wake iliyoandaliwa katika Ikulu.

Katika moja ya mikutano ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa katika mji wa kusini – mashariki wa Masaka, wafuasi walivaa fulana zenye maandishi kama vile ‘Muhoozi K ni rais wetu ajaye’ na ‘Mradi wa MK (MK Project).

Timu mwenyekiti. Nusuru Kesho yako- Secure Your Tomorrow.’ Wengi waliona kuwa huu ulikuwa ni mwanzo wa kampeni ya Muhoozi ya kumrithi baba yake.

Katika dhifa ya kitaifa ya chakula cha jioni ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Muhoozi, Museveni, ambaye alikuwa akikanusha mara kwa mara kumuandaa mwanaye kumrithi alitoa kauli zinazoonyesha kuwa Muhoozi atashika hatamu.

Rais Museveni alinukuliwa na vyombo vya habari vya Uganda akisema, “Muhoozi atapambana na ufisadi, mimi nina subira na watu mafisadi lakini Mohoozi hana subira, atapambana na ufisadi.”

Muhoozi alipandishwa vyeo vya kijeshi haraka na kuingia katika mamlaka ya juu zaidi ya kijeshi, jambo ambalo pia liliibua shutuma kwamba Museveni anamuandaa kwa ajili ya kumrithi.

Katika miaka ya hivi karibuni ametambulika zaidi ndani ya nchi na kimataifa. Kama mshauri wa rais kuhusu operesheni maalumu, cheo alichopata kwa uteuzi na majukumu mengine, Muhoozi alifanya mikutano na viongozi wa Misri, Kenya, Somalia na Rwanda.

Hata hivyo kulingana na katiba ya Uganda wanajeshi hawaruhusiwi kushiriki shughuli za kisiasa nchini Uganda. Iwapo Muhoozi atataka kumrithi baba yake atatakiwa kujiuzulu uanajeshi ili aweze kujitosa rasmi na siasa za uchaguzi.

Je wapinzani wana fursa ya kuiongoza Uganda? Wachambuzi mbali mbali nchini Uganda wanaamini kuwa ni vigumu kwa mtu mwingine yeyote yule tofauti na Museveni na mwanaye Muhoozi wanaweza kuiongoza Uganda wakati Museveni angali bado anataka mamlaka.

"Kwa muonekano na jinsi mambo yalivyo labda utokee muujiza, kwasababu katiba inabadilishwa kila wakati kwa manufaa ya rais Museveni mwenyewe’, anasema mhadhiri Maseruka na kuongeza kuwa.

"Ni sawa na kupigana na mtu mweleka wakati wewe umefungwa kwa pingu."

Maseruka anasema: "Hali ni ile ile ambapo uwanja haujawekwa sawa kidemokrasia na kisheria, awe yoyote yule, awe Kiiza Besigye au Bob Wine wana sifa zote za kugombea, lakini inategemea muamuzi ni nani katika uchaguzi."

Matokeo ya kura za uchaguzi mkuu wa 2021, yalionyesha kuwa kuna idadi kubwa ya waganda wanaotaka mabadiliko ya utawala kinyume na ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.

Kulingana na Tume ya Uchaguzi Uganda (EC) Yoweri Kaguta Museveni alipata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa. Mpinzani wake mkuu , mwanamuziki Bobi Wine, ameshika ambaye alipata nafasi ya pili kwa kupata aliweza kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote - kiasi cha kura ambacho wengi hawakutarajia.

Hivyo basi njia ya Muhoozi ya kufika Ikulu huenda ikawa sio rahisi. Umma wa Waganda utamtarajia ashinde uchaguzi kwa njia halali na huenda punde atakapojitokeza kuwania urais akakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa Bobi Wine ambaye ufuasi wake wa wapiga kura vijana unaendelea kuongezeka.

Chanzo: BBC