Rais wa Uganda Yoweri Museveni amelihutubia bunge la nchi hiyo kwa njia ya mtandao, na kwa mara nyingine tena kupuuzia mbali mbali ripoti za mitandao ya kijamii kwamba alikuwa mgonjwa sana na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Museveni, ambaye alipatikana na Covid-19 wiki iliyopita, Jumatano aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba hana dalili zozote, ingawa vipimo kadhaa alivyofanyiwa vinaonyesha badao ana virusi vya ugonjwa.
Aliwashukuru Waganda ambao wamekuwa wakimuombea na kumtakia uponaji wa haraka.
Alitania kwamba sasa yeye ni "mkongwe wa Corona".
Hotuba yake kupitia njia ya mtandaoni ilikuwa ya kwanza, kwa sababu kama hangekuwa na Covid-19, rais angehutubia bunge wakati wa kusomwa kwa bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha wa 2023-2024.
Waziri wa Fedha Matia Kasaija, ambaye alitoa hotuba ya bajeti, aliambia bunge kwamba uchumi wa nchi unatarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na athari za janga la corona.
Ukubwa wa uchumi sasa unakadiriwa kufikia shilingi trilioni 184.3 za Uganda (kama dola bilioni 50 za Kimarekani) na unatarajiwa kukua kwa kiwango cha asilimia 5.5 katika mwaka wa fedha wa 2023-2024.
Serikali inalenga kubuni nafasi za kazi milioni 2.5 katika miaka mitano ijayo, kulingana na hotuba ya bajeti.
Bw. Museveni alisema kuwa serikali itaendelea kuzingatia miundombinu, uanzishaji wa viwanda, na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa ukuaji wa uchumi.