TUME ya Taifa ya Uchaguzi Uganda imemtangaza aliyekuwa mgombea wa chama cha NRM, Yoweri Museveni kuwa rais wa awamu ya sita kwa ushindi wa asilimia 58.64.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Januari , 14 mwaka huu, Museveni amepata kura 5,851,037. Mwenyekiti wa Tume, Justice Byabakama alitangaza matokeo hayo jana.
Mpinzani mkuu wa Museveni, mwanamuziki Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.
Alisema Mgombea wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Amuriat Oboi alipata kura 323,536 sawa na asilimia 3.24 huku wagombea waliobakia wakipata asilimia chini ya moja.
Museveni mwenye umri wa miaka 76, amekuwa madarakani kwa miaka 35.