Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Museveni amshukuru Samia soko la sukari

F29623807d84ff283aa7a1433a21ef63.jpeg Museveni amshukuru Samia soko la sukari

Thu, 13 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wafanyabiashara wa Uganda wauze sukari Tanzania.

Museveni alisema jana kuwa, Uganda inazalisha sukari tani 600,000 kwa mwaka lakini wanatumia tani 380,000 hivyo wana ziada ya tani 220,000.

Aliyasema hayo baada ya kuapishwa katika kitongoji cha Kololo jijini Kampala ukiwa ni muhula wa sita kwake kuiongoza nchi hiyo. Rais Samia alihudhuria sherehe hizo.

Mbali na shukurani kwa Rais Samia, Rais Museveni pia alimshukuru Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Burundi Everist Ndayishimiye kwa kuruhusu Uganda iuze sukari kwenye nchi hizo.

Tanzania ina uhusiano mzuri na serikali ya Uganda kiasi cha kushirikiana katika miradi mikubwa ya kiuchumi ambayo wataalamu wa uchumi wanaiita kuwa ni injini za uchumi wa mataifa hayo.

Mradi wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Kampala itakayorahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam hadi katika jiji hilo.

Aidha mradi wa pili ni usafiri na usafirishaji katika Ziwa Victoria ambapo meli ya MV Victoria inasafiri hadi Uganda kutoka katika jiji la kibiashara la Mwanza na Bukoba mkoani Kagera.

Mradi wa tatu ujenzi wa bomba la mafuta uliotiwa saini mwezi uliopita ambapo Uganda itasafirisha mafuta kutoka Hoima hadi jijini Tanga.

Rais Yoweri Museveni aliwahi kuishi Tanzania mpaka alipomaliza masomo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na akarudi nchini humo kupigania uhuru wa nchi yake.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo mbali na Tanzania, Burundi na Kenya ni Rais wa Guinea Alpha Conde, Felix Tshisekedi wa DRC, Salva Kiir wa Sudan Kusini, na Ado Akufo wa Ghana.

Wengine ni Heige Geingob wa Namibia, Mohammed Farmajo wa Somalia, na Emmason Mnangagwa wa Zimbabwe, Saleh Zewede wa Ethiopia, Makamu wa Rais wa Nigeria Yemi Osibanjo, Marick Agal, mjumbe wa Baraza la Sudan na Rose Aponda ambaye ni Waziri Mkuu wa Gabon.

Museveni aliapishwa kwa kuwa alishinda katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Januari 14 mwaka huu.

Alitangazwa mshindi kwa kupata kura 5,851,037 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, aliyepata kura 3,475,298.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Uganda, Rais Museveni alipata asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa. Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Simon Byabakama mpinzani wake mkuu akipata asilimia 34.83.

Uchaguzi huo ulikuwa na wagombea 11 wa urais akiwemo mwanamke.

Mgombea huyo kwa tiketi ya chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Amuriat Oboi alikuwa wa tatu, akipata kura 323,536 ambazo ni asilimia 3.24 ya kura zote zilizopigwa.

Mugisha Muntu wa ANT alipata kura 65,334 huku mgombea kwa tikiti ya chama cha DP, Norbert Mao, akipata kura 55,665.

Wengine walikuwa ni John Kabuleta: 44,300, Nancy Kalembe: 37,469, John Katumba: 35,983, Willy Mayambala: 14,657, Fred Mwesigye: 24,673 na Henry Tumukunde, aliyepata kura 50,141.

Chanzo: www.habarileo.co.tz