Rais wa Uganda Yoweri Museveni amejitolea kusaidia kuiunganisha tena Somalia na eneo lake lilolojitenga na kujiita Jamhuri ya Somaliland kaskazini mwa nchi hiyo baada ya kukutana na Mjumbe Maalum wa Somaliland Jama Musse Jama nchini Uganda.
Siku ya Jumamosi Museveni aliandika katika mitandao ya kijamii kwamba: "Nilikubali kuchukua jukumu la mwezeshaji wa amani kati ya pande hizo mbili. Soko la ndani la nchi pekee halitoshi; kwa hiyo, Somaliland na Somalia zinahitaji kuungana, kufanya biashara pamoja, na kufanya biashara na nchi nyingine za Afrika."
Kulingana na kiongozi huyo wa Uganda, kuungana tena kutakuwa na manufaa kwa uchumi na kutakuza ustawi wa wakazi wa eneo hilo.
Rais Museveni alisisitiza kuwa, nchi yake haiungu mkono kujitenga kwa Somaliland kutoka Somalia kwa sababu, kimkakati, ni makosa.
Kwa upande wake, Jama amenukuliwa akisema kuwa Museveni, ambaye amekuwa akiiunga mkono serikali ya Somalia katika mapambano yake dhidi ya magaidii tangu 2007, ni kiongozi muhimu katika mazungumzo ya kuungana tena pande mbili kutokana na ushawishi wake katika Afrika Mashariki.
Rais Yoweri Museveni na Mjumbe Maalum wa Somaliland Jama Musse Jama nchini Uganda Somaliland ilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991 baada kuanguka kwa utawala wa kidikteta wa Mohamed Siad Barre. Jumuiya ya kimataifa inatambua serikali ya shirikisho ya Somalia yenye makao yake makuu mjini Mogadishu kama mamlaka pekee halali nchini humo, lakini sehemu ya kaskazini ya nchi hiyo iko chini ya udhibiti wa serikali isiyotambulika inayojiita Jamhuri ya Somaliland, huku sehemu ya mashariki ya nchi hiyo, eneo la Puntland nalo lijijitangazia mamlaka ya ndani mwaka 1998.
Mwishoni mwa Agosti, wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya Somalia wanaojulikana kama SSC-Khatumo waliripotiwa kukamata kambi mbili muhimu za kijeshi za jeshi la Somaliland karibu na mji wa Las Anod. Mkoa wa Sool na mji wake mkuu wa Las Anod ni eneo linalozozaniwa kati ya Somaliland na Puntland.