Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Museveni: Tutashirikiana na Tanzania kuboresha maisha

Ab9fc1ee91d747e93c782994ff9cba91 Museveni: Tutashirikiana na Tanzania kuboresha maisha

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuboresha maisha ya watu kiuchumi na kisiasa.

Alisema hayo wakati akimshukuru Rais John Magufuli kwa salamu zake za pongezi alizompa baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14, mwaka huu nchini humo.

“Nakushukuru sana Rais Magufuli na watu wote wa Tanzania. Uganda na Tanzania zitaendelea kushirikiana ili kuboresha maisha ya watu wetu kiuchumi na kisiasa,” alisema.

Katika salamu zake za pongezi, Rais Magufuli alisema anampongeza Rais huyo mteule na wananchi wa Uganda kwa uchaguzi wa amani.

“Nakupongeza Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni kwa kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda kuwa mshindi wa kiti cha Urais. Tanzania itaendeleza urafiki na udugu zetu kwa maslahi mapana ya wananchi. Hongereni Waganda kwa kukamilisha Uchaguzi Mkuu, endeleeni kudumisha amani na upendo,” alisema.

Hivi karibuni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Uganda ilimtangaza Museveni aliyekuwa akigombea kupitia chama cha NRM kuwa Rais wan chi hiyo kwa awamu ya sita baada ya kushinda kwa kupata asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa.

Museveni alishinda urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14, mwaka huu kwa kupata kura 5,851,037 ya kura zote zilizopigwa.

Aliyekuwa mpinzani wake mkuu, msanii Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.

Wagombea wengine waluoshiriki uchaguzi huo ni wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) Amuriat Oboi aliyepata kura 323,536 (asilimia 3.24), huku waliobakia wakipata asilimia ndogo chini ya moja.

Chanzo: habarileo.co.tz